Monday, August 18, 2014

Polisi kukomesha unyanyasaji wa kijinsia

photo-2
Na Demetrius Njimbwi – Jeshi la Polisi-Dodoma,
Mkuu wa Dawati la Jinsia Nchini, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Adolfina Chialo, amewataka askari wote nchini hususan wale waliopo katika dawati la jinsia kuhakikisha wanafanya kazi kwa weledi ili kukomesha vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto.
Hayo aliyasema jana wakati akifunga semina ya mafunzo ya siku tano yaliyotolewa  kwa Maafisa na askari wa Jeshi la Polisi pamoja na wadau wa Jeshi hilo katika mkoa wa Dodoma, wilaya ya Kongwa, ambapo washiriki hao wamepatiwa mafunzo ya namna ya kushughulikia makosa ya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji wa watoto.
Kamishna Chialo, alisema kuwa, ili kutokomeza makosa yatokanayo na ukatili wa kijinsia na unyanyasaji kwa watoto, ameihasa jamii kutofumbia macho uovu au aina yeyote ya ukatili na badala yake kuripoti jambo hilo mahala husika au  katika madawati ya jinsia ya Polisi katika kituo chochote cha Polisi  ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa huku akiitaka jamii kuimarisha ulinzi dhidi ya mtoto ikiwa pamoja na malezi bora.
Hata hivyo, akisoma lisala mbele ya mgeni rasmi na kwa washiriki wa semina ya mafunzo  hayo, Albert Bilia, ambaye pia ni mshiriki katika mafunzo hayo amesema kuwa, kutokana na mafunzo waliyopatiwa  yatasaidia zaidi katika kukabiliana na makosa ya ukatili na unyanyasaji ikiwa pamoja na vitendo viovu vinavyofanyika katika jamii husika alisema.
Alisema kuwa, mafunzo haya pia yatasaidia kuongeza weledi uelewa na ufanisi kwa askari Polisi pamoja na wadau wengine walioshiriki mafunzo haya mahakama, waalimu, Ustawi wa jamii pamoja na madaktari, ambao tayari wamezifahamu sheria na mikataba mbalimbali ya kitaifa na kimataifa ikiwa pamoja na sheria ya mtoto ya mwaka 2009 ya Tanzania Bara na sheria ya mtoto ya mwaka 2011 ya visiwani Zanzibar.
Aidha, kamanda wa Polisi mkoani hapa, David Misime, amewataka maofisa pamoja na askari Polisi na wadau waliopatiwa mafunzo haya kuitumia vyema  elimu waliyopewa katika kutanzua na kubaini viashiria vyote vinavyosababisha ukatili kwa jamii  huku akiwaasa wananchi kuachana na mila na desturi zilizopitwa na wakati ambazo kwa kiasi kikubwa zimekuwa zikichangia vitendo vya ukatili na unyanyasaji katika familia alisema.
Kamanda, Misime, aliongeza kuwa, lengo kuu la mafunzo haya ni kujenga uelewa wakati wa kumuhudumia muathiliwa wa ukatili wa kijinsia na unyanyasaji huku akisisitiza suala la utoaji wa huduma bora kwa wateja na kuhakikisha kuwa elimu hiyo inatumika kwa malengo yaliyokusudiwa alisema.

Wanafunzi wawili wa sekondari ya Kamuli Kyerwa wauawa na radi

Na Theonestina Juma, Kagera
WANAFUNZI wawili wa shule ya sekondari Kamuli Wilayani Kyerwa, wamefariki dunia na mmoja kujeruhiwa baada ya kupigwa na radi usiku wakiwa wamelala.

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana mjini Bukoba na kuthibitishwa na Kaimu Mkuu wa shule hiyo, Bw.Marco Renatus   tukio hilo limetokea usiku wa kuamukia Agosti 18, mwaka huu.

Wanafunzi waliofariki dunia wametajwa kuwa ni pamoja na Amon Anaseth mwanafunzi wa kidato cha nne pamona na Onesmo Odilo mwanafunzi wa Kidato cha kwanza katika shule hiyo ya Kamuli.

Aidha aliyejeruhiwa katika tukio hilo ametajwa kuwa ni Filbert Jacksonary ambaye amepatiwa matibabu katika kituo cha afya kilicho wilayani humo na hali yake inaendelea vizuri.

Kwa mujibu wa Makamu wa shule hito, Bw. Marco wakati radi  ikipiga wanafunzi hao walikuwa ndani wamelala.

Alisema radi hiyo imebomoa ukuta wa chumba cha kwanza na cha pili walimokuwa wamelala wanafunzi hao.

Hili ni tukio la pili ndani ya wiki moja ya radi kupiga na kuwauawa raia mkoani hapa katika wilaya ya Karagwe kata ya Kanoni.

Jeshi la Polisi Mkoani hapa limethibitisha kutokea kwa tukio hilo.



Friday, August 1, 2014

Mambo ya Nane Nane Hayoooo 2014

image_5
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Ali Mohamed Shein akiondoka katika Viwanja vya Gongo vya Maonesho ya Nane Nane Kitaifa mara tu baada ya kukamilisha shughuli ya uzinduzi huo leo Agosti 1, 2014 Mkoani Lindi(Picha zote na Lucas Mboje).
photo
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Ali Mohamed Shein(kulia) akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Mkoa wa Lindi Mhe. Agnes Hokororo mapema leo Agosti 1, 2014 alipowasili Viwanja vya Gongo tayari kwa ufunguzi rasmi wa Maonesho ya 21 ya Wakulima na Wafugaji yanayofanyika Mkoani Lindi Kitafa kwa mara ya kwanza tangu yaanzishwe hapa Nchini.
image
Waziri wa Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, Mhe. Dkt. Titus Kamani akitoa Salaam za Wizara katika Maonesho ya Nane Nane Kitaifa kabla ya kumkaribisha Mgeni rasmi, Rais wa Zanzibar Alhaj Dkt. Ali Mohamed Shein(Meza Kuu)katika ufunguzi wa Maonesho hayo ya Wakulima na Wafugaji ambayo yanafanyika Mkoani Lindi Kitaifa.
image_1
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Ali Mohamed Shein(katika Jukwaa) akiwahutubia Wakulima, Wafugaji pamoja na Wananchi wa Mikoa ya Kusini yaani Lindi na Mtwara katika Ufunguzi rasmi wa Maonesho ya Nane Nane Kitaifa yanayofanyika katika Viwanja vya Gongo, Mkoani Lindi leo Agosti 1, 2014.
image_2
Baadhi ya Washiriki mbalimbali wa Maonesho ya Nane Nane Kitaifa wakisikiliza hotuba ya Mgeni rasmi Rais wa Zanzibar, Alhaj Dkt. Ali Mohamed Shein(hayupo pichani). Waliovaa Tisheti za Bluu ni Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza toka Makao Makuu ya Jeshi la Magereza Kitengo cha Kilimo na Mifugo.
image_3
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Ali Mohamed Shein akipata maelezo toka kwa Maafisa Wataalamu wa Benki Kuu ya Tanzania ya namna Wakulima wanavyoweza kupata dhamna ya Mikopo katika Mabenki mbalimbali hapa Nchini kwa Benki Kuu ya Tanzania alipotembelea Banda hilo leo Agosti 1, 2014 katika Sherehe za Maonesho ya Nane Nane Kitaifa yanayofanyika Mkoani Lindi kwa mara ya kwanza.
image_4
Wasanii wa Kikundi cha Utamaduni wakicheza ngoma ya kijadi Maarufu sana Mkoani Lindi.

Waziri Mkuu,Pinda-Karibuni muwekezei Mbeya

PG4A8000
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akifungua kongamano la
uwekezaji  la Nyanda za Juu kusini  kwenye ukumbi wa Mkapa jijini
Mbeya August 1, 2014. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
PG4A8077
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akiongozana na Mkuu wa mkoa wa Mbeya,
Abbas Kandoro  (kushoto) na Mkuu wa WIlaya ya Wanging’ombe,, Esterina
Kilasi  kutoka kwenye ukumbi  wa Mkapa jijini Mbeya  baada  ya
kufungua Kongamano  la Uwekezaji la Kanda ya Nyanda za Juu Kusini
August 1, 2014. (Picha na  Ofisi ya Waziri Mkuu)

Wednesday, July 16, 2014

Hatutatimia BVR Kuhesabu kura tutatumia mikono katika vituo vya kupigia kura-Tume ya Uchaguzi

Na Theonestina Juma, Bukoba
KATIKA kuhakikisha teknolojia mpya ya Biometric Voter Registration (BNR) haileti tatizo,wakati wa kuboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura,Tume ya Uchaguzi imesema italazimika kuweka vituo vyake vya busta.
 Hayo yamebainishwa leo na, Jaji Mkuu Mstaafu wa Zanzibar ambaye pia ni  Kamishna wa Tume ya Uchaguzi Taifa, Hamid Mahamoud wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Bukoba.
 “Mfumo wa BVR ulileta shida kubwa kwa nchi ya Kenya, lakini kwetu sisi tumejipanga kikamilifu katika kukabiliana na tatizo hili, ikiwa ni pamoja na kutotumia mtandao mmoja wa simu, tutalazimika hata kuweka vituo vya busta ili taarifa zetu ziweze kwenda kama inavyotarajiwa”alisema.
 Jaji Hamid alisema mfumo wa BVR kwa upande wao Tume ya kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura watautumia kwa kazi mmoja tu ya kuboresha daftari la wapiga kura na si vinginevyo.
 “Sisi tumedhamiria kutumia mfumo wa BVR kwa ajili ya kuboresha daftari la wapiga kura tu, mambo ya kuhesabu kura tutatumia njia yetu ya kawaida ambayo ni kuhesabu kwa mikono katika vituo vya kupigia kura na wasimamizi kusaini kama ilivyo desturi yetu”alisema.
 Alisema katika mfumo huo ambao watachukua alama za vidole 10 vya mikono, picha na saini kwa wale watakaojiandisha ambapo kwa upande wa walemavu wasiokuwa na vidole vya mikono watapigwa picha na kuchukuliwa sura zao kama walivyo.
 “Mtu asiyekamilika atachukuliwa jinsi alivyo kwani ni haki yake, atapigwa picha”alisema Jaji Hamid.
 Halikadhalika alibainisha kuwa kabla ya kuanza zoezi la uboreshaji wa daftari hilo la wapiga kura ambalo linatarajiwa kuanza Mwezi Septemba mwaka huu unaweza kuchukua takribani miezi mitatu hadi kukamilimka kwake, kuna mkoa mmoja ambao umeteuliwa kwa ajili ya kufanyia majaribio ya vifaa vitakavyotumika.
 Hata hivyo, Jaji Hamid hakuwa tayari kuutaja mkoa huo kwa maelezo kuwa utatajwa hapo baadaye.
 Kuhusu wahamiaji haramu kupenyeza kujiandikisha katika daftari hilo, aliwataka wananchi kuwa na uthubutu na kuwataja majina ya watu ambao wanaamini kuwa si raia wakiwa na uthibitisho.
 Alisema baada ya uboreshaji wa daftari hilo majina yatabandikwa sehemu ya wazi ili kuwawezesha wananchi kuwabaini wahamiaji haramu waliojiandikisha ili waweze kuondolewa majina yao katika orodha hilo.
 Aliwataka wananchi siku ikifika wajitokeze kwa uwingi ili kujiandikisha upya hata kwa wale wenye kadi zao za zamani na wale  ambao hawana kwa vile hizo kadi za zamani hazitatumika katika upigaji kura katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwakani.
 Pia aliwataka vijana ambao watatimiza miaka 18 Septemba mwakani nao wajitokeze katika kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura.

Mwisho.

Saturday, July 12, 2014

CCM Missenyi yahodhi majengo 14 ya serikali ya vijiji, wananchi walia

Na Theonestina Juma, Missenyi

MGOGORO mkubwa unafurukuta kati ya baadhi ya wananchi na Chama cha mapinduzi Wilaya ya Missenyi ya kugombania majengo 14 ya vijiji yaliyojengwa na serikali kupitia mfuko wa Kagera Rehabilitation baada ya vita vya Kagera mwaka 1978/1979 yanayohodhiwa na CCM hadi sasa.

Hayo yamebainika jana baada ya kundi la wananchi wapatao 10 wa kijiji cha Bulifani kata ya Kyaka wilyani humo kuandama hadi ofisi ya Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Missenyi, Bi Elizabeth Kitundu kulalamikia baadhi ya viongozi wa kijiji hicho waliotakiwa kuendesha mkutano wa kijiji ulioitishwa kisheria kukimbia kusiko julikana na kuwaacha wananchi peke yao.

Katika mkutano huo, wananchi hao wakitaka kuelezwa hatima ya jengo lao linalomikiwa na CCM  na kuwapangisha wafanyabishara mbali mbali ikiwemo Benki ya NMB tawi la Missenyi, ambapo kodi wanalipwa CCM na serikali ya kijiji haiambulii chochote huku wananchi wakichangishwa sh.40,000 kwa kila mwananchi kwa ajili ya ujenzi wa shule za kata.

Hatua hiyo inatokana na baada ya Chama cha Demokrasia na Mandeleo (Chadema) Wilaya ya Missenyi kuibua suala hilo tangu miaka miwili iliopita ambapo kwa sasa mgogoro huo unaonekana kufukuta moshi, baada ya baadhi ya wananchi ambako majengo hayo yamejengwa katika vijiji vyao kuelewa kuwa majengo hayo ni mali yao na si ya CCM.

Hata hivyo  inaelezwa kuwa chanzo cha fukuto hilo, kwa mujibu wa Barua ya Katibu wa CHADEMA wilaya ya Missenyi iliosainiwa na Bw. Ilidephonce Vedasto yenye kumbu kumbu namba CDM/MIS/ADM/VOL.1/16 kwenda kwa Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Missenyi  ni baada ya uongozi wa CCM tawi la Bulifani kumwandikia barua Mwenyekiti wa serikali ya kijiji Bulifani kata ya Kyaka, Bw. Deogratius Kahwa kuwa hapaswi kuingia katika jengo la CCM kwa sababu anatokana na Chama cha CHADEMA.

Katika tamko lao CHADEMA kimetoa siku 14 kwa Mkurugenzi huyo kuhakikisha kuwa kinaondoa CCM katika majengo hayo, siku ambazo zimeisha Julai 10, na kimetishia kumshtaki mahakamani kwa kushirikiana na CCM kuhujumu mali za umma.

halika nguvu ya umma itatumika kukiondoa CCM katika majengo hayo ambapo watawahamasisha umma ukate mawasiliano na dhidi ya Mkurugenzi .

Bw. Vedasto alisema katika barua hiyo kuwa, halmashauri hiyo imeshapoteza mapato mengi yatokanayo na majengo hayo ambapo bila kujua uongozi wa halmashauri hiyo imekuwa ikiwalipia pango la ofisi za Watendaji wa vijiji kwa CCM, majengo husika ni mali ya serikali ya kijiji.

Hata hivyo kwa mujibu wa barua kutoka katika ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Bukoba ambayo ndiyo ilikuwa wilaya mama kabla kuundwa kwa wilaya ya Missenyi, yenye kumbu kumbu namba KGR/BDC/S.2/51/49 kwenda kwa Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Missenyi, Bi.Kitundu inathibitisha kuwa majengo hayo ni mali ya wananchi.

Katika barua hiyo iliosainiwa na  P.Magesa kwa niaba ya Mkurugenzi wa halmashauri hiyo ilieleza kuwa majengo ya ofisi za vijiji yaliojengwa baada ya vita vya Nduli Iddi Amin, mwaka 1978/1979 yalijengwa kwa lengo la kurekebisha miundo mbinu iliyoharibiwa na vita hivyo.

Aidha ililenga kuboresha mazingira ya wakazi wa Tarafa ya Missenyi kwa wakati huo ambapo serikali ilitekeleza sheria ya vijiji ya Namba 21 mwaka 1975 kuhusu ofisi za vijiji.

“Kwa kuwa muundo wa serikali ulikuwa ni chama Kimoja ndani ya majengo hayo kuliwekwa Katibu wa vijiji kwa sasa ni Mtendaji wa Kijiji , Afisa elimu Watu Wazima kwa sasa wanajulikana kama Afisa Mtaribu elimu Kata, duka la kijiji na ukumbi wa mkutano”ilisema sehemu ya barua hiyo.

Hata hivyo, baada ya majengo hayo kukamilika mfuko huo uliendelea kujenga madarasa ya shule za msingi nne Kakiri pamoja na nyumba za walimu mbili kwa moja (two in one) madarasa 25 ya shule za msingi katika maeneo ya Bugorora, Irango, Ruhunga, Kimkunda na Mabuye na vitabu vya kusoma na kufundishia katika shule mbali mbali zipatazo 40.

Halikadhalika malambo ya maji yalichimbwa katika kata ya Kilimilile, Kyamulaile na Kakunyu , pamoja na ujenzi wa MCH Kakiri na kituo cha zahanati ya Byeju.

Katika barua hiyo iliendelea kueleza kuwa majengo hayo hayakujengwa kwa ajili ya CCM bali kwa ajili ya serikali za vijiji na hakuna barua ya makabidhiano ya majengo hayo kwa CCM kwamba kilichopo ni hati ya uandikishaji wa vijiji na maduka ya Ushirika ya mwaka 1975.

Hata hivyo, kwa upande wa Mkurugenzi wa wilaya hiyo, Bi. Kitundu alisema kuwa mazungumzo yanafanyika ili kuweza kuangalia namna ya kufanya ikiwemo kushirikisha uongozi wa wilaya ambaye kwa sasa yuko likizo.
Mwisho.

Friday, June 20, 2014

Mahakama ya mkoa Kagera yawafuta kazi madiwani saba wa Manispaa ya Bukoba

Na Theonestina Juma, Bukoba
 MADIWANI sita  kati ya tisa waliokuwa wanashtakiwa kwa kosa la kushindwa kududhuria vikao vya vya Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera wamevuliwa vyadhifa zao na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Kagera.

Akisoma hukumu hiyo leo mbele ya Mahakama hiyo,Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Charles Uiso, alisema madiwani hao wanavuliwa udiwani huo kutokana na mahakama hiyo kuidhika na ushahidi wa pande ushahidi uliotolewa mahakamani hapo.

Ilielezwa mahakamani hapo kuwa madiwani hao,walikuwa wakikataa kuhudhuria vikao vya baraza la madiwani pamoja na vikao mbali mbali vya baraza hilo jambo lilisababisha kurudisha nyuma  maendeleo ya wananchi wa manispaa ya Bukoba.

 Uiso amesema kuwa ushahidi wote uliotolewa mahakamani hapo umeweza kuridhisha mahakama bila kuwa na shaka lolote.

Madiwani waliovuliwa nafasi zao za udiwani ni pamoja na Bw. Samuel Ruangisa kata Kitendaguro(CCM) Bw.,Deusdedith Mutakyahwa kata Nyanga(CCM,),Bw.Yusuph Ngaiza kata Kashai(CCM),Bw.Dauda Kalumuna kata Ijuganyondo (CC) , Bi. Murungi Kichwabuta Viti maalumu(CCM)na Rabia Badru viti maalumu (CUF).

Hata hivyo, mahakama hiyo imetupilia mbali malalamiko dhidi ya madiwani wengine wawili Bw. Richard Mwemezi kata Miembeni(CCM)na Bw.Israel Mlaki kata Kibeta(CHADEMA) kwa madai kuwa  hawa hawahusiki moja ka moja na malamiko hayo kwani na kwa Bw.Richard kuwa  hakuwa mjumbe wa kamati hiyo na Israel Mraki aliweza kuhudhuria baadhi ya vikao hivyo.

 Kutokana na hali hiyo  Mahakama imewaamuru madiwani hao saba  waliovuliwa  udiwani kulipa gharama za uendeshaji wa kesi hiyo kwa mlalamikaji.

Hukumu ya kesi hiyo iliyotumia takribani masaa mawili, ilivuta hisia za watu na kuwafanya wagawanyike katika pande mbili zilizowahusu wafuasi wa mbunge wa jimbo la Bukoba mjini Hamis Kagasheki(CCM) na aliyekuwa Meya wa Manispaa hiyoDkt.  Anatory Amani,ambavyo mvutano wa makundi hayo yalianza kuibuka mara tu baada ya kuwepo malumbano dhidi ya vigogo hao wa kisiasa.

kesi hiyo ilifunguliwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Afya, elimu na uchumi Bw.Chief Kalumuna, ambaye pia ni diwani wa kata Kahororo(CCM)  ambapo madiwani hao ambao walikuwa wajumbe wa kamati yake walikaidi  kuhudhuria vikao zaidi ya tano.

Alitaja baadhi ya vikao walivyotakiwa kukaa na tarehe kuwa ni pamoja na   Julai 19, Agosti 1,septemba 23,novemba 11 na novemba 14 mwaka 2013.

MWISHO