Na Theonestina Juma, Bukoba
KATIKA kuhakikisha teknolojia
mpya ya Biometric Voter Registration (BNR) haileti tatizo,wakati wa kuboreshaji
wa daftari la kudumu la wapiga kura,Tume ya Uchaguzi imesema italazimika kuweka
vituo vyake vya busta.
Hayo yamebainishwa leo na, Jaji
Mkuu Mstaafu wa Zanzibar ambaye pia ni Kamishna wa Tume ya Uchaguzi Taifa, Hamid
Mahamoud wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Bukoba.
“Mfumo wa BVR ulileta shida
kubwa kwa nchi ya Kenya, lakini kwetu sisi tumejipanga kikamilifu katika
kukabiliana na tatizo hili, ikiwa ni pamoja na kutotumia mtandao mmoja wa simu,
tutalazimika hata kuweka vituo vya busta ili taarifa zetu ziweze kwenda kama
inavyotarajiwa”alisema.
Jaji Hamid alisema mfumo wa
BVR kwa upande wao Tume ya kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura
watautumia kwa kazi mmoja tu ya kuboresha daftari la wapiga kura na si
vinginevyo.
“Sisi tumedhamiria kutumia mfumo
wa BVR kwa ajili ya kuboresha daftari la wapiga kura tu, mambo ya kuhesabu kura
tutatumia njia yetu ya kawaida ambayo ni kuhesabu kwa mikono katika vituo vya
kupigia kura na wasimamizi kusaini kama ilivyo desturi yetu”alisema.
Alisema katika mfumo huo
ambao watachukua alama za vidole 10 vya mikono, picha na saini kwa wale
watakaojiandisha ambapo kwa upande wa walemavu wasiokuwa na vidole vya mikono
watapigwa picha na kuchukuliwa sura zao kama walivyo.
“Mtu asiyekamilika
atachukuliwa jinsi alivyo kwani ni haki yake, atapigwa picha”alisema Jaji Hamid.
Halikadhalika alibainisha
kuwa kabla ya kuanza zoezi la uboreshaji wa daftari hilo la wapiga kura ambalo
linatarajiwa kuanza Mwezi Septemba mwaka huu unaweza kuchukua takribani miezi
mitatu hadi kukamilimka kwake, kuna mkoa mmoja ambao umeteuliwa kwa ajili ya
kufanyia majaribio ya vifaa vitakavyotumika.
Hata hivyo, Jaji Hamid hakuwa
tayari kuutaja mkoa huo kwa maelezo kuwa utatajwa hapo baadaye.
Kuhusu wahamiaji haramu
kupenyeza kujiandikisha katika daftari hilo, aliwataka wananchi kuwa na
uthubutu na kuwataja majina ya watu ambao wanaamini kuwa si raia wakiwa na
uthibitisho.
Alisema baada ya uboreshaji
wa daftari hilo majina yatabandikwa sehemu ya wazi ili kuwawezesha wananchi
kuwabaini wahamiaji haramu waliojiandikisha ili waweze kuondolewa majina yao
katika orodha hilo.
Aliwataka wananchi siku
ikifika wajitokeze kwa uwingi ili kujiandikisha upya hata kwa wale wenye kadi
zao za zamani na wale ambao hawana kwa
vile hizo kadi za zamani hazitatumika katika upigaji kura katika uchaguzi mkuu
unaotarajiwa kufanyika mwakani.
Pia aliwataka vijana ambao watatimiza
miaka 18 Septemba mwakani nao wajitokeze katika kujiandikisha katika daftari la
kudumu la wapiga kura.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment