Na Theonestina Juma, Missenyi
MGOGORO mkubwa unafurukuta kati ya baadhi ya wananchi na Chama cha mapinduzi Wilaya ya Missenyi ya kugombania majengo 14 ya vijiji yaliyojengwa na serikali kupitia mfuko wa Kagera Rehabilitation baada ya vita vya Kagera mwaka 1978/1979 yanayohodhiwa na CCM hadi sasa.
Hayo yamebainika jana baada ya kundi la wananchi wapatao 10 wa kijiji cha Bulifani kata ya Kyaka wilyani humo kuandama hadi ofisi ya Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Missenyi, Bi Elizabeth Kitundu kulalamikia baadhi ya viongozi wa kijiji hicho waliotakiwa kuendesha mkutano wa kijiji ulioitishwa kisheria kukimbia kusiko julikana na kuwaacha wananchi peke yao.
Katika mkutano huo, wananchi hao wakitaka kuelezwa hatima ya jengo lao linalomikiwa na CCM na kuwapangisha wafanyabishara mbali mbali ikiwemo Benki ya NMB tawi la Missenyi, ambapo kodi wanalipwa CCM na serikali ya kijiji haiambulii chochote huku wananchi wakichangishwa sh.40,000 kwa kila mwananchi kwa ajili ya ujenzi wa shule za kata.
Hatua hiyo inatokana na baada ya Chama cha Demokrasia na Mandeleo (Chadema) Wilaya ya Missenyi kuibua suala hilo tangu miaka miwili iliopita ambapo kwa sasa mgogoro huo unaonekana kufukuta moshi, baada ya baadhi ya wananchi ambako majengo hayo yamejengwa katika vijiji vyao kuelewa kuwa majengo hayo ni mali yao na si ya CCM.
Hata hivyo inaelezwa kuwa chanzo cha fukuto hilo, kwa mujibu wa Barua ya Katibu wa CHADEMA wilaya ya Missenyi iliosainiwa na Bw. Ilidephonce Vedasto yenye kumbu kumbu namba CDM/MIS/ADM/VOL.1/16 kwenda kwa Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Missenyi ni baada ya uongozi wa CCM tawi la Bulifani kumwandikia barua Mwenyekiti wa serikali ya kijiji Bulifani kata ya Kyaka, Bw. Deogratius Kahwa kuwa hapaswi kuingia katika jengo la CCM kwa sababu anatokana na Chama cha CHADEMA.
Katika tamko lao CHADEMA kimetoa siku 14 kwa Mkurugenzi huyo kuhakikisha kuwa kinaondoa CCM katika majengo hayo, siku ambazo zimeisha Julai 10, na kimetishia kumshtaki mahakamani kwa kushirikiana na CCM kuhujumu mali za umma.
halika nguvu ya umma itatumika kukiondoa CCM katika majengo hayo ambapo watawahamasisha umma ukate mawasiliano na dhidi ya Mkurugenzi .
Bw. Vedasto alisema katika barua hiyo kuwa, halmashauri hiyo imeshapoteza mapato mengi yatokanayo na majengo hayo ambapo bila kujua uongozi wa halmashauri hiyo imekuwa ikiwalipia pango la ofisi za Watendaji wa vijiji kwa CCM, majengo husika ni mali ya serikali ya kijiji.
Hata hivyo kwa mujibu wa barua kutoka katika ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Bukoba ambayo ndiyo ilikuwa wilaya mama kabla kuundwa kwa wilaya ya Missenyi, yenye kumbu kumbu namba KGR/BDC/S.2/51/49 kwenda kwa Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Missenyi, Bi.Kitundu inathibitisha kuwa majengo hayo ni mali ya wananchi.
Katika barua hiyo iliosainiwa na P.Magesa kwa niaba ya Mkurugenzi wa halmashauri hiyo ilieleza kuwa majengo ya ofisi za vijiji yaliojengwa baada ya vita vya Nduli Iddi Amin, mwaka 1978/1979 yalijengwa kwa lengo la kurekebisha miundo mbinu iliyoharibiwa na vita hivyo.
Aidha ililenga kuboresha mazingira ya wakazi wa Tarafa ya Missenyi kwa wakati huo ambapo serikali ilitekeleza sheria ya vijiji ya Namba 21 mwaka 1975 kuhusu ofisi za vijiji.
“Kwa kuwa muundo wa serikali ulikuwa ni chama Kimoja ndani ya majengo hayo kuliwekwa Katibu wa vijiji kwa sasa ni Mtendaji wa Kijiji , Afisa elimu Watu Wazima kwa sasa wanajulikana kama Afisa Mtaribu elimu Kata, duka la kijiji na ukumbi wa mkutano”ilisema sehemu ya barua hiyo.
Hata hivyo, baada ya majengo hayo kukamilika mfuko huo uliendelea kujenga madarasa ya shule za msingi nne Kakiri pamoja na nyumba za walimu mbili kwa moja (two in one) madarasa 25 ya shule za msingi katika maeneo ya Bugorora, Irango, Ruhunga, Kimkunda na Mabuye na vitabu vya kusoma na kufundishia katika shule mbali mbali zipatazo 40.
Halikadhalika malambo ya maji yalichimbwa katika kata ya Kilimilile, Kyamulaile na Kakunyu , pamoja na ujenzi wa MCH Kakiri na kituo cha zahanati ya Byeju.
Katika barua hiyo iliendelea kueleza kuwa majengo hayo hayakujengwa kwa ajili ya CCM bali kwa ajili ya serikali za vijiji na hakuna barua ya makabidhiano ya majengo hayo kwa CCM kwamba kilichopo ni hati ya uandikishaji wa vijiji na maduka ya Ushirika ya mwaka 1975.
Hata hivyo, kwa upande wa Mkurugenzi wa wilaya hiyo, Bi. Kitundu alisema kuwa mazungumzo yanafanyika ili kuweza kuangalia namna ya kufanya ikiwemo kushirikisha uongozi wa wilaya ambaye kwa sasa yuko likizo.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment