Sunday, October 5, 2014

Wakurugenzi na Maafisa elimu ambao ni walimu ndiyo vinara wa kuwanyanya walimu wenzao nchini-Pinda

Na Theonestina Juma, Kagera

Serikali imesema inaendelea kuboresha maslahi ya walimu nchini licha ya kukabiliwa na changamoto kubwa ya kiuchumi.

Hayo yamesemwa leo na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwa niaba ya Rais wa Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete, wakati akihutubia katika kilele cha maadhimisho ya siku ya mwalimu duniani yaliofanyika katika Manispaa ya Bukoba.

Alisema kulingana na hali halisi ya walimu ndiyo inayoongoza kuwa na watumishi wengi katika kada zote hapa nchini, serikali inaendelea kuwaboreshea maslahi yao kulingana na hali ya uchumi wa nchi.

Halikadhalika Waziri Pinda aliahidi serikali kuwachukulia hatua kali za kisheria watumishi wa Halmashauri walioo ngeza takwimu katika madeni ya walimu wanaoidai serikali.

“Hawa watumishi walioamua kuingiza madeni hewa kwa kuongeza tarakimu mbele, lazima watafutwe na kuchukuliwa hatua kwa kuisababishia serikali hasara, kwani mwalimu mwenyewe anajua anadai serikali kiasi gani..”alisema.


Alisema Serikali ilibaini kuwepo kwa madai hewa ya sh.bilioni10.9,sh. billion 9 kutoka TAMISEMI na sh. bilioni 1.5 kutoka wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi baada ya kukosa  viambatanisho  na vielelezo vya kuthibitisha uhalali wa madai hayohivyo kuonekana ni batili.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu alionesha kusikitishwa na  vitendo vinavyofanywa na baadhi ya wakuu wa idara wanaopandishwa vyeo kutokea sekta ya elimu kuwanyanyasa walimu wenzao pindi wanapohitaji msaada.

Alisema “ utendaji usioridhisha unasababishwa na baadhi ya walimu waliobahatika wakapata nafasi za Ukurugenzi na Afisa elimu kutowasikiliza walimu wake wakati matatizo yao wanayafahamu kwa nini hawa watu wanakuwa na roho mbaya kama hii”.

“Baadhi  ya Maafisa elimu ndio matatizo na taabu kwa walimu hawawezi kupitisha fomu za malipo ya uhamisho hadi wapewe hongo wakati na yeye ametoka huko huko… ni jambo la kusikitisha”aliongeza

Alisema walimu wanapofunga ndoa na kuomba kuwafuata wenzi wao wamekuwa wakizungushwa bila sababu za msingi.

“Kuna mambo mengine ni ya kushangaza waliotakiwa kuwasaidia walimu ndio wanageuka kuwa mbogo, mtu unamzungusha weee… hutaki amfuate mumewe hivi ni hawara yako?... hiyo ni roho mbaya” ninaikemea

Naye Naibu Waziri wa elimu na mafunzoya ufundi Bi.Jenister Muhagama, alisema sera ya elimu imeshakamilika itazinduliwa na Rais wowote na kwamba itahakikisha kuwa walimu wanaendelezwa kielimu.

Halikadhalika alibainisha kuwa bodi ya fani ya ualimu na Tume ya utumishi yameridhiwa na serikali kuanzishwa na ifikapo mwakani yatakuwa tayari kuanza kazi.
  
Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Alhaji Yahya Msulwa,alitoa zaidi ya mapendekezo 11 kwa ili kuwezesha kuboresha taaluma ya ualimu na maslahi ya watumishi na sekta ya elimu kiujumla.

Miongoni mwa mapendekezo hayo ni pamoja na serikali kurejesha posho ya ufundishaji kwani walimu ndiyo wanafanya kazi muda mrefu kuliko mtumishi yeyote hapa nchini na duniani kijumla.

Pia aliiomba serikali kuwajengea walimu nyumba za kulala kwa kushirikiana na wawekezaji kama Shirika la Nyumba  ambapo alibainisha kuwa kwa sasa kuna upungufu wa nyumba za walimu nchini 109,560 wakati nyumba zilizopo ni 55,000.

Halikadhalika aliiomba serikali kuwashirikisha kikamilifu walimu katika mabadiliko ya mitaala, kwani yanapofanyika bila kuwashirikisha walimu huaathiri kutokana na wao ndiyo watekelezaji wakuu wa mitaala hiyo.


mwisho

No comments:

Post a Comment