Sunday, October 5, 2014

Siasa za Bukoba zamsikitisha Waziri Mkuu

PIX 3.WAZIRI MKUU Mizengo Pinda ameutaka uongozi wa mkoa wa Kagera ukae na kuzungumza ili kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa kisiasa katika Manispaa ya Bukoba kwa manufaa ya wananchi.
Ametoa wito huo jana usiku wakati akizungumza na viongozi na watendaji wa Serikali wa mkoa huo mara baada ya kupokea taarifa ya mkoa huo iliyowasilishwa kwake na Mkuu wa Mkoa huo, Kanali (Mst) Fabian Massawe.
Waziri Mkuu aliwasili Bukoba jana jioni akitokea Dodoma ili kumwakilisha Rais Jakaya Kikwete kwenye maadhimisho ya Siku ya Walimu Duniani ambayo kitaifa yanafanyika mkoani Kagera
Waziri Mkuu Pinda alisema: “Ninatumaini viongozi mtakaa na kuzungumza na kukubaliana kuondoa kesi mahakamani ili kazi za kusaidia wananchi zifanyike…. Wewe kiongozi si kitu chochote, wenye kustahili kupewa uzito ni wananchi,” alisema.
Alisema anaumizwa na viongozi wa mkoa huo kukosa uchungu kwa kuwanyima wakazi wa manispaa hiyo uwezo wa kupata maendeleo kwa ajili ya mtu mmoja.
“Kuna hela zimetolewa na Benki ya Dunia kiasi cha sh. bilioni 18/- lakini zitapotea hivi hivi kwa sababu ya maslahi binafsi ya watu wachache. Pesa za maendeleo zinatakiwa zifanyiwe maamuzi katika vikao, lakini watu hawawezi kukutana sababu ya mtu mmoja.”
“Kuna fedha za maendeleo zinazotolewa na Serikali na ili zitumike ni lazima zipitishwe kwenye vikao lakini bila kujali maslahi mapana ya watu mtu anaenda mahakamani na kuzuia kila kitu kisifanyike hadi matakwa yake yatimizwe.”
Mapema, akiwasilisha taarifa ya mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali (Mst) Fabian Massawe alimweleza Waziri Mkuu kwamba tatizo la kisiasa katika Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba bado linaendelea
Mkuu huyo wa mkoa alisema hivi sasa kuna zuio la mahakama (court injuction) la kutofanyika kwa vikao katika halmashauri lilitolewa Agosti 25, 2014 hadi hapo kesi namba 2/2014 iliyopo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Bukoba itakapohitimishwa.
Alisema kesi nyingine mbili bado zinaendelea mahakamani baada ya kesi ya kutaka madiwani sita wavuliwe udiwani kutolewa hukumu mnamo Juni 25, 2014.
“Kuna kesi ya rufaa namba 11/2014 katika Mahakama Kuu ya Tanzania – Bukoba ya Mhe. Yusufu G. Ngaiza na wenzake watano dhidi ya Chifu Adronicius Kalumuna na Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba, wakipinga uamuzi wa kuondolewa udiwani. Rufaa hiyo ilipokelewa Julai 18, 2014 na imepangwa kusikilizwa tarehe 13 Oktoba, 2014,” alisema.
Kesi ya pili ni kesi namba 02/2014 iliyopo Mahakama ya hakimu Mkazi Bukoba ya Mhe. Anatory Amani ya kutaka Mkurugenzi wa Manispaa amtambue kuwa yeye ni Meya wa Manispaa hiyo na kumpatia haki na stahiki zake. Kesi hii ilifunguliwa Agosti 12, 2014 na imepangwa kuanza kusikilizwa Oktoba 6, mwaka huu.
Alimweleza Waziri Mkuu kwamba kulikuwa na kesi nyingine namba 01/2014 katika Mahakama Kuu ya Mhe. Anatory Amani dhidi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na mwanahseria Mkuu wa Serikali ambayo ilifunguliwa Machi 7, mwaka huu ambapo mlalamikaji alitaka mambo kadhaa kuhusiana na taarifa ya ukaguzi maalum iliyotolewa Januari 17, 2014 yatenguliwe na mahakama.
 “Aliiomba mahakama itengue taarifa hiyo kuwa batili na isitambulike kisheria lakini mahakama imeiondoa kesi hiyo tarehe 25 Septemba, 2014 kwa kuwa ilipelekwa mahakamani hapo chini ya kifungu kisicho sahihi,” alisema

No comments:

Post a Comment