Na Theonestina Juma, Kemondo Bay
ABIRIA 381 waliokuwa wakisafiri na Meli ya Mv. Victoria kutoka Bukoba kuelekea Jijini Mwanza wameingia na taharuki kubwa baada ya meli hiyo kuzimika ghafla ziwani.
Katika tukio hilo abiria hao inadaiwa kuwa walianza kunyanyang'anya maboya huku kukiwa hakuna hata mfanyakazi mmoja melini aliyejitokeza kuwatangazia wachukue tahadhari gani wala kuwatuliza.
Kutokana na hali hiyo, nahodha wa meli hiyo alijitahidi kuikokota meli hiyo hadi bandari ndogo ya Kemondo ambapo abiria wote walilazimika kulala hapo bila kujua hatima yao.
Meli hiyo ilizimika usiku wa kuamukia Oktoba 11 mwaka huu saa 6:00 usiku ambapo si kawaida meli hiyo kuwasili katika bandari ya Kemondo kwa muda huo.
Kwa mujibu wa baadhi ya abiria waliokuwa wakisafiri na meli hiyo waliondoka bandari ya Bukoba majira 3.00 usiku kama ilivyo kawaida ya meli hiyo na kufika kemondo saa 6:00 badala ya saa 4:30 hadi saa 5:00.
Bw.Gervas Mugisha, alisema wakati wanaondoka bandari ya Bukoba baada ya mwendo wa saa moja waliona Meli ikianza kupoteza mwelekeo muda mfupi baadaye ilizimika na tena kuanza safari bila kutangaziwa kitu chochote na watumishi wa meli hiyo.
Alisema"tukiwa bado hatujafika Kemondo Meli ilizimika mara tatu hali hiyo iliwatia hofu abiria na kuanza kukimbilia maboya na kunyang’anyana hadi kufikia hatua ya kuyachana ili kila mtu akose"
Hata hivyo kutokana na hali hiyo walilala bandari yake mondo bila kupewa maelekezo yoyote kulipopambazuka wananchi waliokuwa safarini waliamua kujimwaga katika barabara kuu iendayo Mwanza wakishinikiza uongozi wa meli hiyo kuwarejeshea nali zao.
Nahodha wa meli hiyo, Bw.Bembere Samson alisema tatizo lililotokea ni kufeli kwa mfumo wa umeme na kusababisha kupoteza mweleko kwa muda wa dakika10.
Bw.Samson, alisema tatizo la mfumo wa meli hiyo haihitaji matengenezo makubwa bali inahitaji kubadilisha kifaa ambacho kilitarajiwa kuletwa na ndege kutoka jijini Mwanza.
Hata hivyo alisema kuwa, kuchelewa kufika kwa meli kwa wakati unategemeana uzito wa mizigo uliobebwa ndani ya meli na sio ubovu.
Alisema, meli hiyo inauwezo wakubeba abiria 1200 lakini jana ilikuwa na abiria 381 na inauwezo wakubeba tani 200 za mizigo bila kubainisha kwa jana walikuwa wamebeba tani ngapi za mizigo.
Naye Afisa Mfawidhi wa Mamalaka ya Uthibiti wa Usafirishaji wa Majini na nchi Kavu (SUMATRA ) Kapteni Alex Katama, alisema meli hiyo haina hitilafu yoyote lakini tatizo lililojitokeza ni la kawaida tu.
"Meli hiyo iko salama tatizo lililotokea ni la kawaida sio ajabu mfumo wa umeme ndio ulioleta hitilafu"alisema.
Alisema kulingana na utaratibu na kanuni za sumatara chombo chochote kinacho tumia Injini mbili hakiwezi kuruhusiwa kuendelea na safari kwa kutumia Injini moja.
Alisema, meli hiyo ya Mv Victoria ina mfumo wa kisasa wa kuongoza meli kwa kutumia umeme, waliotoka Bukoba kwa kutumia mfumo mbadala na ndio maana walilazimika kutia nanga katika bandari ya Kemondo kwa usalama wa Abiria.
Hata hivyo baadaye meli hiyo ilitengemeaa na abiria kuendelea na safari zao kuelekea Jijini Mwanza.
No comments:
Post a Comment