Sunday, October 5, 2014

Pinda ni aibu kata moja kuwa na maprofesa zaidi ya 40 na wanafunzi wa eneo hilo kukosa madawati

DSCF3243*Yanahitajika madawati 99,204 kwa shule zote za msingi
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda ameutaka uongozi wa mkoa wa Kagera ulichukulie suala la upungufu wa madawati kwa uzito ule ule kama ilivyo kwenye suala la ujenzi wa maabara katika shule za sekondari.
Ametoa wito huo jana usiku (Jumamosi, Oktoba 5, 2014) wakati akizungumza na viongozi na watendaji wa Serikali wa mkoa huo mara baada ya kupokea taarifa ya mkoa huo iliyowasilishwa kwake na Mkuu wa Mkoa huo, Kanali (Mst) Fabian Massawe.
Waziri Mkuu aliwasili Bukoba jana jioni akitokea Dodoma ili kumwakilisha Rais Jakaya Kikwete kwenye maadhimisho ya Siku ya Walimu Duniani ambayo kitaifa yanafanyika mkoani Kagera.
“Kwenye ujenzi wa maabara naona mnafanya vizuri lakini nataka kwa uzito uleule tusimamie suala la upungufu wa madawati. Tuunganishe nguvu za wananchi wa kawaida na za Serikali za Mitaa ili kuondoa kabisa tatizo hili mkoani mwenu,” alisema.
“RC hapa kasema kuna kata moja huko Bugandika kuna maprofesa 40. Huwezi kuwa na Maprofesa wote hao halafu kwenye shule wanakotoka maprofesa hao eti watoto wanakaa chini, haiwezekani!” alisisitiza.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ofisi ya Katibu Tawala wa mkoa huo, mkoa wa Kagera unahitaji madawati 238,080 kwa shule zote za msingi ambapo yaliyopo ni 138,876 na upungufu ni madawati 99,204. Kwa shule za sekondari, mkoa unahitaji viti 84,344, vilivyopo ni 82,275 na pungufu ni 2,069 wakati mahitaji ya meza ni 84,344; zilizopo ni 73,615 na upungufu ni 10,729.  
Aliwataka viongozi wa mkoa huo watafute mbinu za kukuza kipato cha wananchi wanaowaongoza kama njia mojawapo ya kuwasaidia wananchi wao kujikwamua kiuchumi. “Kwanza jiulize pato la mkoa likoje na limeongezeka kiasi gani? Je hali ya watu wangu ikoje? Nifanye nini ili niweze kuwaondoa hapo walipo na kuwafikisha katika kiwango kingine cha maendeleo?” alisisitiza
Alisema kama kila kiongozi atadhamiria kupambana na umaskini wa kipato wa wananchi, ni dhahiri kuwa kazi ya kuondoa maadui wengine ambao ni maradhi na ujinga itakuwa rahisi mno.
Mapema, akiwasilisha taarifa ya mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali (Mst) Fabian Massawe alisema mkoa huo unahitaji kujenga maabara 570 ambapo zilizopo ni 136 wakati zingine 434 ziko katika hatua mbalimbali za ujenzi. Alisema mkoa unatumia maabara zinazohamishika (mobile labs) ambazo zipo 35.
Aliosema mkoa huo pia unazo hosteli za wananfunzi 84 na unahitaji kujenga hosteli nyingine 212 ili kuwasaidia watoto wa kike waweze kuhitimu masomo yao.
Akizungumzia hali ya ulinzi na usalama mkoani humo, Kanali Massawe alisema kati ya Desemba 2013 na Septemba 2014, jumla ya wahamiaji haramu 1,589 kutoka nchi jirani za Burundi, Rwanda Uganda na DRC wameondoshwa nchini na wengine 231 waliondoka kwa hiari ikiwa ni utekelezaji wa Operesheni Kimbunga Endelevu.
“Katika operesheni Kimbunga ya awali wahamiaji 25,258 waliondolewa nchini ikiwa ni sawa na asilimia 48 ya wahamiaji wote 50,520 wanaokadiriwa kuwepo mkoani Kagera. Tangu wakati huo, tumeendelea na misako kwenye mabasi, maeneo ya starehe, nyumba za kulala wageni, viwandani, mashambani, taasisi za elimu, taasisi za madhehebu ya kidini, vipenyo na vijiji vya mpakani.”
“Kuanzia Januari hadi Septemba mwaka huu, jumla ya watu 572 walikamatwa na kufikishwa mahakamani au kufukuzwa nchini (PI). Walioshtakiwa walikuwa ni 431 na kuhukumiwa vifungo ama kutozwa faini na wahamiaji 231 walifukuzwa nchini kwa PI,” alifafanua.

No comments:

Post a Comment