Friday, October 10, 2014

Mwalimu wa shule ya sekondari Kagemu avamiwa kanisa usiku wa manane auawa kwa mapanga


Na Theonestina Juma, Bukoba

WATU wasiojulikana wamevamia Kanisa usiku wa manane na kumuua kikatili  mwalimu wa shule ya sekondari ya Kagemu kwa kumcharanga mapanga hadi kufa huku mtu mwingine akikatwa mguu wa kushoto.

Mauaji hayo ya kikatili yamefanyika ndani ya kanisa  la Pentekoste Assemblies of God ( PAG ) iliko katika Kata ya Kitengaguro usiku wa manane mwalimu huyo pamoja na wenzake wakiwa kwenye mkesha wa maombi kanisani humo.

Mwalimu aliyeuawa kikatili kiasi hicho amejulikana kuwa ni Bw. Dionis Ng’wandu ambaye wauaji hao walimcharanga mapanga sehemu za kichwani na kufariki dunia papo hapo.

Aidha aliyekatwa mguu wa kushoto amejulikana kwa jina moja la Bw. Themistocles  fundi ujenzi .
 
Kwa mujibu wa  Mchungaji wa kanisa hilo, Faustine Joseph, alisema baadhi ya waumini wa kanisa hilo wanadesturi ya kuomba hadi saa nne usiku.

Alisema kwa siku hiyo baada ya maombi waliamua kuondoka  majira ya saa 5:00 usiku  na kumuacha marehemu Bw. Ng’wangu  na mwenzake wakiendeleana mkesha wa maombi. 

Mchungaji Joseph,alisema  tukio hilo lilitokea  saa 8.00 usiku  ambapo alipigiwa simu  usiku huo na majirani wa eneo wanaoishi karibu na kanisani hapo.

'Nilipigiwa simu na mmoja wa majirani wa kanisa letu kuhusu watu wasiojulikana kuvamia waliokuwa kwenye maombi ya mkesha, nilipofika niliwakuta polisi wameshafika... kwa kweli hali inatisha sana"alisema.

Alisema katika uvamizi huo ambao ndiyo mara ya kwanza kutokea kanisani hapo watu hao hawakuiba kitu chochote hata simu zao walizokuwa nazo zaidi ya kufanya ukatili huo wa kutisha.

Hata hivyo, habari zaidi zinadai kuwa chanzo cha uvamizi huo unahusishwa na imani za kidini kwamba waliohusika na tukio hilo ni wapinzani wa dini hiyo.

Inadaiwa kuwa hadi wanatendewa kitendo hicho wahusika walikuwemo peke yao  majira ya saa 8 usiku baada ya wenzao kuondoka bada saa 4 usiku hivyo wao waliamua kulala kanisani.

Habari hizo zinadai kuwa mauaji ya mwalimu huyo yametokea  baada ya kuoa mwanamke wa dini nyingine na kumbadilisha dini.

Hatu hiyo inadaiwa kuwa iliwahudhi waumini wa dini ya mkewe ambao walianza vitimbi kwa kanisa hilo.

Kamanda wa polisi Mkoa wa kagera, Henry Mwaibambe ,alithibitisha kutokea kwa tukio hilo .
Alisema mwili wa mwalimu Ng'wangu umehifadhiwa katika hospitali ya mkoa Kaagera huku majeruhi wa tukio hilo amelazwa katika hospitali ya Mkoa Kagera kwa matibabu zaidi.

Alisema mtu mmoja ambaye hakuwa tayari kutaja jina lake anashikiliwa na Jeshi hilokwa mahojiano zaidi ambapo watu watatu wanatafutwa .



No comments:

Post a Comment