Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete (kushoto) akikabidhiwa Katiba Inayopendekezwa toka kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Mhe. Samuel Sitta wakati wa sherehe ya Makabidhiano ya Katiba hiyo iliyofanyika jana 08 Oktoba, 2014 mjini Dodoma.
…………………………………………………………………..
Na Benedict Liwenga, Maelezo-Dodoma.
KATIBA Inayopendekezwa imekabidhiwa rasmi 8 Oktoba, 2014 kwa Waheshimiwa Marais wa Tanzania Bara, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete pamoja Rais wa Zanzibar, Mhe. Ali Mohammed Shein.
Akihutubia wakati wa sherehe ya Makabidhiano ya Katiba hiyo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alisema kuwa tukio hilo la kukabidhiwa Katiba Inayopendekezwa ni jambo la kihistoria kwa nchi ya Tanzania na linaashiria kukamilika rasmi kwa kazi ya lililokuwa Bunge Maalum la Katiba lililoanza tarehe 18 Februari mwaka huu.
Mhe. Dkt. Kikwete alisema kuwa ni hatua nyingine ya kihistoria ya nchi kwani hatua ambayo imesalia hivi sasa ni ile ya wananchi kwenda kuipigia kura za maoni Katiba hiyo ili waweze kufanya uamuzi kuhusiana na Katiba hiyo na endapo wananchi hao wataikubali basi Tanzania itakuwa imejipatia Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Sina budi Kumshurkuru Mwenyezi Mungu kwa hapa tulipofikia na sina budi kumshukuru Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Mhe. Samuel John Sitta, Makamu wake Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya, nawashukuru pia Wenyeviti wa Kamati mbalimbali za Bunge Maalum kwa uongozi waa makini, natoa pia shukurani za pekee kwa Wajumbe wote wa Bunge Maalum la Katiba kwa kukamilisha kazi hii tena mmeikamilisha kazi hii kwa kiwango cha juu sana cha ubora”, alisema Mhe. Dkt. Kikwete.
“Shukurani zangu pia ziende kwa Katibu wa Bunge Maalum na Naibu Katibu pamoja na Wasaidizi wao wote kwa kazi nzuri walioifanya na kuiwezesha Bunge Maalum la Katiba kukamilisha kazi yake kwani haikuwa kazi rahisi hata kidogo”, aliongeza Mhe. Dkt. Kikwete.
Naye Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Dkt. Ali Mohammed Shein alimpongeza Rais wa Tanzania Bara, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuanzisha mchakato huo wa kupata Katiba mpya na alitoa pongezi zake kwa Mwenyekiti wa lililokuwa Bunge Maalum la Katiba, Mhe. Samule Sitta pamoja na Makamu wake Mhe. Samia Suluhu ikiwemo pongezi pia kwa Wajumbe wote walioshiriki katika mchakato huo.
Katika Hotuba yake, Mhe. Dkt. Shein alisema kuwa katika mchakato mzima wa kutafuta Katiba hiyo, Zanzibar ilishirikishwa kikamilifu kwani hakuna hata hatua moja ambayo haikushiriki.
“Nataka leo nisisitize kuwa Zanzibar ibaki sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kila hatua ya mchakato huu imeshirikishwa na kushiriki kikamilifu hadi hivi leo tulipofikia”, alisema Dkt. Shein.
Naye aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi wa lililokuwa Bunge Maalum la Katiba. Mhe. Andrew Chenge alisema kuwa ndani ya Katiba hiyo katika eneo la Uongozi, kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania imeweka Ukomo wa idadi ya Mawaziri pamoja na Naibu Mawaziri ambapo kwa mapendekezo hayo, idadi ya Mawaziri na Naibu Mawaziri haitazidi 40.
Mhe. Chenge alifafanua kuwa idadi hiyo ya Mawaziri na Naibu Mawaziri itaisadia Serikali na Wananchi kupunguza gharama kwa ujumla na pia katika suala hilo hilo la uongozi aliongeza kuwa Rais wa Zanzibar anapokuwa Makamu wa Rais ni ishara ya Muungano, hivyo itaisadia Serikali ya Jamhuri ya Muungano kudumisha Muungano uliopo.
Aidha, Katika masuala yanayohusu Bunge, Chenge ameeleza kuwa Katiba inayopendekezwa inapendekeza mambo mawili ya msingi ambayo ni Uwiano wa Wabunge pamoja na Ukomo wa Idadi yao.
“Kuhusu Uwiano wa Wabunge, inapendekezwa kuwepo na uwiano ulio sawa kati ya Wabunge Wanaume na Wabunge Wanawake uwe asilimia hamsini kwa hamsini”, alisema Chenge.
Akiongea kuhusu suala la ukomo wa Wabunge hao, wote wa kuchaguliwa na wale wa kuteuliwa, Mhe. Chenge alibainisha kuwa idadi hiyo haitapungua 340 na haitazidi 390.
“Mhe. Rais, Katiba hii Inayopendekezwa imesheheni malengo muhimu, ya Kiuchumi, ya Kisiasa, kijamii, ya kiutamaduni na kimazingira”, alisema Chenge.
Aliongeza kuwa katika malengo ya Taifa na kijamii yameboreshwa zaidi kwa kuweka mazingira yatakayowezesha Wasanii pamoja na Wanamichezo kukuza na kuendeleza vipaji vyao na kuleta mabadiliko ya kiuchumi katika jamii.