Licha
ya kuwa ni siku ya huzuni kwa dunia nzima, hotuba ya Rais wa Marekani,
Barack Obama imewagusa maelfu ya watu waliokuwa kwenye Uwanja wa FNB
katika ibada ya kitaifa kumwaga Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson
Mandela.
Obama
aliyetumia dakika 20 katika hotuba yake iliyokuwa ikikatizwa na kelele
za kumshangilia, aliwataka vijana wa Afrika na dunia nzima kuiga maisha
aliyoishi Mandela kama yeye alivyojifunza mambo mengi kutoka kwa
mzalendo huyo.
“Miaka
30 iliyopita nikiwa mwanafunzi, nilisoma Kitabu cha Mandela na tangu
siku hiyo nilijifunza, nikajenga roho ya uthabiti. Iliamsha uwajibikaji
kwa ajili yangu na kwa ajili ya watu wangu… hakika Mandela amenifanya
niwe hivi nilivyo leo. Michelle na mimi tumenufaika sana na Mandela,”
alisema Obama na kuongeza:
“Mandela
alinifanya niwe mtu ninayesimama mbele yenu leo, alichangia kunifanya
kuwa kiongozi bora. Nitaendelea kuiga mfano wake,”
Katika
sherehe hizo, Obama alipokewa kwa shangwe na kushangiliwa kila
alipopita na kila alipozungumza tofauti na ilivyokuwa kwa Rais wa nchi
hiyo, Jacob Zuma ambaye alikuwa akizomewa.
Obama
alimtaja Mandela kama kiongozi anayefaa kuigwa kwani pamoja na kukaa
gerezani kwa miaka 27 akipigania uhuru, hakutaka kung’ang’ania madaraka
na badala yake alistaafu kwa hiari yake, tofauti na viongozi wengi wa
Afrika.
“Mandela
alionyesha uongozi wa vitendo na kujaribu, alikuwa ni mwanamume,
binadamu wa kawaida, mume, baba na kiongozi shupavu,” alisema Obama.
Pia
Obama alisema, Mandela aliachiwa huru kama mfungwa, lakini kama mwalimu
ambaye alitumika kutuonyesha kuwa, ni lazima kuwaamini wenzako ili nao
wakuamini.
“Kufundisha
upatanisho, hakuhitaji kudharau historia mbaya ya nyuma bali ni
kuikabili kwa umakini, ukweli na uhalisia wake. Mandela alibadili
sheria, lakini alibadili mioyo yetu pia,” alisema.
Katika
risala hiyo, Obama alimtaja Mandela kama mwanamapinduzi mkubwa wa karne
ya 20 aliyeibadilisha mioyo ya watu wake, akaimarisha mapatano na
maelewano kwa wazungu na weusi.
“Amezaliwa
kipindi cha Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, kijana aliyekuwa akichunga
ng’ombe na kuteswa na wakubwa zake wa kikabila, lakini ameibuka na kuwa
mwanamapinduzi mkuu wa karne ya 20,” alisema Obama.
Vilevile,
Obama alimfananisha Mandela na Abraham Lincoln, Rais wa zamani wa
Marekani kwa kuiunganisha nchi yake pale ilipokuwa inataka kuvurugika.
Rais
huyo aliufanya umati katika uwanja huo ulipuke zaidi kwa furaha baada ya
kuzungumza neno la Kizulu, ‘ubuntu’ linalomaanisha utu au ubinadamu
ambapo alisema Mandela ameimarisha utu na ubinadamu kwa Waafrika Kusini.
“Alidumisha
‘utu’ miongoni mwetu. Utu ambao tunaweza kuupata kwa kushirikiana na
kuwajali wanaotuzunguka,” alisema Rais huyo ambaye anatajwa kuwa Rais wa
dunia. Obama alionyesha umahiri wake katika risala hiyo na katika
sehemu ya risala hiyo alisema ni wajibu wa kila mmoja kuiga maisha
aliyoishi Mandela.
“Ni lazima tujifunze kutoka kwake, kwa sababu Waafrika Kusini kwa jumla wao wameonyesha kuwa, tunaweza kubadilika.”
Obama
alimtaja Mandela kama mtu asiyependa kujikweza bali aliyeshiriki
kuonyesha mawazo yake na hofu na uhalisia wake hasa kwa kusema kuwa yeye
si mtakatifu labda kama mtakatifu ni sawa na mwenye dhambi ambaye
hachoki kujaribu. Kiongozi huyo alimalizia hotuba hiyo kwa nukuu muhimu
za Mandela zinazosema kuwa, ‘Mimi ni kiongozi wa imani, mustakabali
wangu, na mimi ni nahodha wa roho yangu’ na kuwataka Waafrika Kusini
kuishi katika maneno hayo ya Mandela katika maisha yao.
“Hakika
ilikuwa roho ya ajabu, tutamkumbuka sana. Mungu wabariki Waafrika
Kusini,” alimaliza Obama. Kabla ya hotuba hiyo, Obama alifanya jambo la
kihistoria kwa kupeana mikono na Rais wa Cuba, Raul Castro, kama ishara
ya mapatano baada ya migogoro iliyoko baina ya nchi hizo mbili.
Kabla
ya Obama kuzungumza, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon katika
hotuba yake alisema kuwa, alijitoa muhanga kwa ajili ya usalama, uhuru
na demokrasia ya nchi yake.
“Sherehe
hizi za kumbukumbu zinadhihirisha upinde wa mvua wa taifa. Ninatumaini
tutaweza kuuona upinde huo punde, kupitia mvua ya simanzi,” alisema
Ki-Moon. Ki-Moon alimtaja Mandela kuwa ni kiongozi aliyejiandaa kupoteza
kila kitu kwa ajili ya uhuru na demokrasia.
“Dunia
imepoteza rafiki na mwalimu. Alikuwa ni zaidi ya viongozi wakubwa wa
nyakati zetu; mwalimu mkuu aliyetufundisha kwa mifano,” alisema Ki-Moon.
Wakati
huo huo, Mkuu wa Majeshi wa nchi hiyo, Jenerali Thanduxolo Mandela kwa
niaba ya familia ya Mandela alipata nafasi ya kutoa risala yake kwa Rais
huyo na alisema kuwa, familia hiyo ina bahati ya kuwa na mzazi kama
Mandela.
“Utakumbukwa daima, hatuwezi kuusahau mchango wako katika familia na katika maisha ya Waafrika Kusini wote,” alisema Thanduxolo.
Baada
ya Thanduxolo, walikuja wajukuu na vitukuu wa Mandela kwa niaba ya
wajukuu wote, Pumla, Andile na Mbuso Mandela ambao walisema wana mengi
waliyojifunza kwa babu yao ambaye walimtaja kuwa kioo cha familia na
kuahidi kuwa wataishi na matendo yake.
Mandela atazikwa Jumapili.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment