Tuesday, December 31, 2013

Kanisa Katoliki Ngara latishia kusitisha kuwabatiza watoto wa kiume

Na Theonestina Juma, Ngara
UONGOZI wa Kanisa Katoliki Parokia ya
Ngara Mjini umetishia waumini wake kusitisha kuwabatiza watoto wao wa kiume wasipobadilika katika kuwabagua watoto wao katika kuwajenga kiimani.

 Tishio hilo limetolewa jana na Paroko wa Kanisa Katoliki la Mtakatifu Fransisco wa Asizi Parokia ya Ngara Mjini, Ivus Tindyebwa wakati akihubiri kanisani hapo ikiwa ni siku ya familia ilioenda sanjari na ubatizo wa watoto zaidi ya 40.
 Kwa jinsi hali ilivyo katika malezi ya  watoto,wazazi wengi wamekuwa wakiwalea watoto wao kimfumo dume, watoto wa kike wakiwa ndiyo wanawajibishwa zaidi huku watoto wa kiume wakiwa hawahimizwi hata kidogo kujishughulisha na masuala ya dini.
 Hatua ya Paroko huyo kusema hayo ni kutokana Jumamosi Desemba 28, mwaka huu jimbo la Rulenge liliadhimisha siku ya utoto Mtakatifu,
wilayani Biharamulo na cha kushangaza watoto wa kike ndiyo walikuwa wengi kana kwamba siku hiyo ilikuwa ni utoto wa usichana."

 "Itafikia hatua sasa siku ya utoto mtakatifu tutabadili iwe siku ya usichana mtakatifu, kwa sababu siku hiyo inayowalenga watoto wa jinsi zote na si watoto wa kike pekee"alisema Paroko huyo.
Aidha  alihoji sababu ya waumini wa kanisa hilo kuegemea kwa watoto wa kike pekee na kuendelea kutoa malezi ya kiroho kiubaguzi uliojaa mfumo dume?
Hata hivyo alisema tatizo la kutoa malezi ya kiroho kiubaguzi haliko wa Jimbo la Runge tu bali ni tatizo kwa nchi nzima na hivyo ni wajibu wa waumini wa kanisa hilo kubadilka katika malezi ya watoto wao kiroho.
 Alisema "wakristo wanatakiwa kubadili mfumo wa ulezi wa watoto wao kiroho kwa kuwahusisha watoto wa jinsi nzote".
 Alisema licha ya wakati wa ubatizo hata majina ya watoto wa kiume yanakuwepo lakini anashangaa ikifika wakati wa huduma kanisani watoto wa kiume hawajitokezi na badala yake watoto wa kike ndiyo wanaonekana wengi.
 Katika hatua nyingine Paroko huyo aliwakata vijana wa kanisa hilo kuachana na ndoa za kuwavuta kwa nguvu wasichana kwani inawafanya kuingia katika sakramenti hiyo bila kuchunguzana, kama wamekomaa kiakili na kimwili katika kulea familia yao kiroho.
Alisema wale wanaoingia katika ndoa kwa mfumo huo mwishoe ndoa yao inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo kutengana baada ya kujigundua kuwa hawawezi kuishi pamoja, jambo ambalo ni changamoto kwa kanisa.
 

No comments:

Post a Comment