Friday, May 10, 2013

Serikali kupambana na kundi ndogo la wachochezi wa kidini nchini-Pinda

http://www.fullshangweblog.com/wp-content/uploads/2013/05/IMG_0607.jpg
WAZIRI mkuu Mh. Mizengo Pinda amesema Serikali ina kazi kubwa ya kushughulika na kundi dogo linalojihusisha na lugha za uchochezi wa kidini ambao unachangia kudhoofisha amani ya nchi.
“Tunajua nia yao ni kufanya nchi isitawalike lakini sisi tumesema hatukubali. Tumekubaliana na Waziri wa Mambo ya Ndani, ulinzi uimarishwe kila mahali, msishangae kuona watu wanawahoji lakini kwa nia njema, ya kurudisha amani yetu,” Alisema mheshimiwa Pinda.
Mh. Pinda Ametoa kauli hiyo leo wakati akiwasilisha salamu za rambirambi kwa niaba ya Serikali wakati wa ibada ya mazishi ya waumini watatu wa Kanisa la Mt. Joseph Mfanyakazi,
Parokia ya Olasiti, jijini Arusha waliofariki dunia kutokana na
mlipuko wa mabomu uliotokea Jumapili iliyopita, Mei 5, mwaka huu kanisani hapo.
Waziri Mkuu amewaomba wanachi kutoka ushirikiano kwa vyombo vya dola kwa kutoa taarifa zozote zitakazosaidia kwenye upelelezi wa tukio hilo.
“Ninawaomba Watanzania tushirikiane kuwafichua watu hawa waovu kwa sababu tunaishi nao, ni watu ambao wako miongoni mwetu… Tusaidieni kutunong’oneza ili tuchukue hatua”, . Alisisitiza mh. Pinda.
Waziri Mkuu alisema yeye ni miongoni mwa watu wanaoamini kwamba ukristo au uislamu hauwezi kuondolewa kwa kuwaua viongozi wa dini au waumini wao. “Ni kujidanganya tu mtu akiamini kuwa akimuua Askofu,Mufti au  Muumini ataimaliza dini yoyote. Madhehebu haya mawili ni nguzo kubwa kwa Taifa letu, tunatamani tuendelee kuwa na amani iliyokuwepo siku zote,” alisisistiza Mh. Pinda.
 Alisema Serikali kupitia idara ya maafa itatoa sh. milioni 100/- ili zisaidie kukabiliana na janga lililowakabili wana Arusha.
Mapema, akiongoza ibada hiyo, Muadhama Polycarp Kardinali Pengo aliwataka waumini wote kutolipa uovu kwa uovu bali watende wema ili kusahihisha maovu. “Ishara ya uovu imetendwa na hawa watu dhidi ya waumini wenzetu kwa madhumuni yanayojulikana na wao tu bila kuchokozwa
na hawa marehemu ama wale waliko hospitali (majeruhi),” alisema.
“Uovu umeshatendwa, je sisi tufanye nini? Angekuja hapa kanisani Yule aliyesababisha mauti haya, tungemfanya nini?” Alihoji Kardinali Pengo na kujibiwa na mamia ya waumini waliohudhuria ibada hiyo: “Tungemsamehe.”
Aliwasihi waumini wote kuendelea kuliombea Taifa la Tanzania ili tukio hilo na lile la kuuawa kwa Padre Evarist Mushi kule Zanzibar yasiwe sababu ya kusambaratika kwa amani ya Taifa hili.
“Tusilipe ubaya kwa ubaya, tuendelee kuomba Mungu asikie sala yetu na awazindue wenye mamlaka watimize wajibu wao,” alisema.
Naye Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Alex Malasusa akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Jukwaa la Wakristo Tanzania (TCF), alilaani waliosababisha mauaji hayo na kusema kitendo hicho kimelitia doa Taifa kwa vile ni kitendo kinachoashiria kuchafua amani ya Tanzania.
Aliwasihi waumini wote kutokuwa waoga katika kazi ya kumtangaza Kristo. “Risasi zinapigwa, mioto inayowashwa katika makanisa yetu na mabomu yanayolipuliwa yasiwe sababu ya kututia hofu. Imani yetu haiku katika miili bali iko mioyoni mwetu,” alisema.
Askofu Mkuu Josephat Lebulu wa Jimbo Kuu la Arusha akitoa shukrani kwa
niaba ya Kanisa Katoliki aliwashukuru wote waliofika kuwafariji
kutokana na tukio hilo na kuwathibitishia kuwa kama Kanisa wameguswa
na moyo waliouonyesha.
Watu 66 waliathirika kutokana na mlipuko huo uliotokea Mei 5, mwaka huu ambapo watatu wamefariki dunia na kati ya wagonjwa 63 waliobakia, wanane walihamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili, wengine waliotibiwa na kuruhusiwa kurudi nyumbani, na baadhi wanaendelea kupatiwa matibabu
mjini Arusha.

No comments:

Post a Comment