Wednesday, May 15, 2013

Huzuni kwa wauza magazeti Kagera , waondokewa na kipenzi chao, Bw. Benezeth



Na Theonestina Juma, Kagera
WAUZAJI wa magazeti katika Manispaa ya Bukoba, Mkoani Kagera wamepata pigo kubwa baada ya mwenzao  Bw. Benezeth Kamigan Barnabas (47) kufariki dunia baada ya kuugua ghafla ugonjwa wa kuoza sehemu ya utumbo mpana.
Kijana wa marehemu, Bw. Benson Kamigan aliyekuwa akimuuguza baba yake katika hospitali ya Mkoa Kagera katika wodi namba moja alikokuwa amelazwa, alisema baba yake alikata roho  jumanne wiki hii, Mei 14, mwaka huu saa 11 jioni mara baada ya kufanyishwa mazoezi ya kutembea.
Alisema baba yake alikimbizwa katika hospitali ya Mkoa Kagera, Mei 2 mwaka huu  usiku wa manane baada ya kulalamikia kusokotwa na tumbo la ghafla.
Alisema kutokana na hali hiyo, Mei 3, mwaka huu baba yake alifanyiwa uchunguzi na kugundulika kuwa kipande cha utumbo wake mpana umeoza.
Hivyo siku hiyo alifanyiwa upasuaji mkubwa wa kuondolewa kipande wa utumbo huo uliokuwa na urefu wa nusu mita.
Hata hivyo, tangu baba yake afanyiwe upasuaji huo, upumuaji wake ulikuwa wa kuhema hema, kwani ilionekana wazi kuwa pumzi ulikuwa si wa kutoka ndani ya tumbo zaidi ya kifuani pekee.
Jumanne wiki hii hali ya baba yake ilibadilika ghafla mara baada ya kutoka kumfanyisha mazoezi ya kutembea kulingana na maelezo aliokuwa akipewa na madaktari kwa ajili ya kujiandaa kuondolewa nyuzi ambapo jioni saa 11 mara tu baada ya mazoezi alikata roho.
“Jioni hii nilikuwa namfanyisha baba mazoezi ya kutembea, lakini tuliporea ndani ya wodi alilala kitandani mara akaanza kutokwa mapovu mdomoni na kutapatapa  kama dakika 15 hivi na kisha akakata roho”alisema Bw. Benson.
Bw. Benezeth aliwahi kuwa wakala wa magazeti ya kampuni ya Business Times Ltd kati ya mwaka 1996  mkoani Kagera na baadaye mwaka 2003 alianza kujikita rasmi katika uuzaji wa magazeti.
Marehemu anatarajiwa kusafirishwa kesho kwenda kuzikwa kijijini kwake Bulembo kata ya Kamachumu Wilayani Muleba.
Bw. Benezeth ameacha mjane watoto saba wakike wakiwa wanne na kiwemo mtoto mchanga wa miezi mitatu na wakiume wakiwa ni watatu.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment