Saturday, November 17, 2012

Wananchi muda wa kufungwa viongozi wetu pingu na kuletwa mbele yetu ni enzi za wakoloni


Na Theonestina Juma, MISSENYI
KITENDO cha Jeshi la polisi Wilayani Missenyi, kumfunga pingu Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mutukula, Bw.Hamidu Mugarula na kuanza kumzungusha mtaa mzima kwa  ajili ya kumtaka awaoneshe wananchi aliowauzia maeneo kwa ajili ya kufanyiabiashara kimezua mapambano makubwa kati ya polisi na wananchi hadi kusababisha polisi kupiga risasi kadhaa hewani na mabomu la machozi
Tukio hilo la aina yake lililoonekana kama sinema na kuwalazimu baadhi a wanachi kukimbia upande wa Uganda kujiokoa kilitokea hivi karibuni (Novemba 6) mwaka huu saa 8 mchana katika eneo la Mutukula mpakani mwa Tanzania na Uganda.
Mapambano hayo yaliodumu kwa saa 5 ililazimu polisi wengine  kuitwa kutoka mjini Bukoba, kwenda kuongeza nguvu ambapo muda huo wote shughuli za biashara na usafirishaji katika eneo hilo la mpakani zilisimama.
Wakizungumza  na gazeti hili,  baadhi ya wananchi na wafanyabishara walioshuhudia tukio hilo walisema chanzo cha mapambano hayo kati ya polisi na wananchi ni baada ya wananchi kuchukizwa na kitendo cha kiongozi wao akiwa amefungwa pingu huku akiwa ametangulizwa mbele na polisi akizungushwa mtaa mzima wakimtaka awaoneshe watu aliowakatia risiti za kuuziwa maeneo kwa ajili ya kufanyia biashara.
Walisema kutokana na hali hiyo, kuliibuka mzozo mkubwa kati ya polisi na wananchi hao, ambao waliwasihi polisi kumfungua pingu kiongozi wao kama wanataka waongee nao.
Alisema wananchi hao walidai kuwa kiongozi wao hawezi kuletwa mbele yao akiwa amefungwa pingu kama mwizi wakati alikuwa akifanya kazi za serikali.
Kutokana na hali hiyo, huku jeshi la polisi, wakiwa hawaelewani na wananchi hao, kwa hasira walianza kufanya vurugu ikiwa ni pamoja na kuwarushia mawe polisi waliokuwa na mwenyekiti huyo, ambapo polisi walipoona hali ni mbaya walilazimika kumbeba mwenyekiti huyo kama ng’ombe na kumtumbukiza ndani ya gari waliokuwa nao na kumkimbiza katika kituo cha polisi cha Kyaka.
Hata hivyo, kitendo hicho kinaelezwa kuwa kilionesha kuzidi kuwakasirisha wananchi hao, na kuamua kukimbia kwenda kufunga kizuizi na kuanza kupanga matairi kwa lengo la kutaka kuharibu gari la polisi ili kumtoa kiongozi wao.
Polisi waliwawahi kupita eneo hilo, ambapo baada ya kuona polisi hao wameondoka na kiongozi huyo, walihamishia hasira zao  kwenye mali za serikali .
Wananchi hao  walivamia ofisi ya kijiji cha Mutukula na kung’oa mlango na madirisha  na kuchoma moto bendera ya Chama cha mapinduzi (CCM) kilichokuwa kikipepea maeneo hayo na kisha kuhamia katika jengo lililokuwa likitumia na halmashauri ya missenyi kwa ajili ya kukatia ushuru na kuliteketeza kwa moto pamoja na nyaraka zote zilizokuwemo.
Mwenekiti wa Katibu wa soko na wafanyabiashara katika eneo hilo la Mutukula, Bw. Theophil Kaembe akizungumza na gazeti hili alisema  katika eneo la Mutukula, kuna eneo lililotengwa na serikali kwa ajili wa ujenzi wa kituo cha mabasi ambapo eneo hilo kutokana na kukaa wazi muda mrefu, huku wananchi wakihangaikia  kutafuta sehemu pa kufanyia biashara,mwenyekiti huyo kwa kushirikiana na Mtendaji wa Kata, Bw.Mukasa Mugarula waliamua kuwagawawia wananchi hao.
Alisema maeneo hayo waligawa kwa kulipia sh. 10,000 ambapo walielezwa kuwa maeneo hayo wamegawawiwa kwa muda kutokana na eneo hilo  ni la serikali na linaweza  kuhitajiwa kwa matumizi aliolengwa kwa muda wowote.
Bw. Kaembe alisema “hata risiti tulizokatiwa zimeandikwa kuwa ni kwa muda si za kudumu, risiti walizozitumia ni ya halmashauri namba HW5”.
Mapambano hao ambayo ililazimika polisi kutolewaa mjini Bukoba kwenda kuongeza nguvu kutuliza ghasia hizo, ilivutia hisia za viongozi, wa mkoani hapa, ilimlazimu hadi Kamanda wa polisi Mkoani hapa, Phillip Kalangi na Mkuu wa wilaya hio, Issa Njiku kufika eneo hilo.
Hata hivyo, Kamanda Kalangi akizungumzia vurugu hizo, alisema kuwa imetokana na malalamiko yaliotolewa na baadhi ya wananchi kuwa wanatakiwa warudishe maeneo hayo wakati waliuziwa kati ya sh. 200,000 hadi 350,000.
Alisema pamoja na vurugu hizo kutokea na kusababiasha shughuli nyingi za kibiashara kusimama kwa muda lakini tayari walishafanya mazungumzo na wananchi wa maeneo hayo na nchi jirani na kusawazisha na hivyo hali imerudi ya kawaida.
Alisema viongozi hao wanaoshikiliwa na jeshi hilo wanatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote, kwa tuhuma a kutumia ofisi ya na wameuziwa maeneo na viongozi wa serikali kutumia vibaya ofisi ya serikali.
mwisho

No comments:

Post a Comment