Monday, November 26, 2012

Bomu lazua tafrani Ngara

Na Theonestina Juma, Bukoba
WANANCHI  wanaoishi karibu na uwanja wa ndege katika  kijiji cha  Ruganzo kata ya Kibimba wilayani Ngara wamegubikwa na hofu kubwa baada ya kitu kizito mithili ya bomu inayotoa hewa ya gesi  ambayomtu akivuta anapiga chafya kudondoka chini kwa kishindo kutoka juu na kusababisha milipuko mingi kutokea.
Tukio hilo la aina yake na ya mara ya kwanza kutokea wilayani humo ambalo linapakana na nchi zaidi ya nne za Afrika Mashariki lilitokea Novemba 22 mwaka huu saa 8 usiku wakati wananchi wakiwa wamelala.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Mkuu wa wilaya ya Ngara, Costantine Kanyasu alisema kitu hicho mfano wa chuma lenye umbo kama la yai  linalotoa hewa ya gesi lilipodondoka chini kwa nguvu na kusababisha  mtikisiko mkubwa wilayani humo jambo lililochangia wananchi kujawa na hofu kubwa.
Alisema pamoja na kutokea milipuko zaidi ya mara tatu wilayani humo haijajulikana kama yamesababishwa na kudondoka kwa chuma hicho ambacho hadi sasa hakijathibitishwa kama ni bomu.
Alisemakutokana na kuwepo sintofahamu kwa wananchi wanaoishi karibu na eneo hilo la uwanja wa ndege, kamati ya ulinzi na usalama umewashauri wananchi kukaa mbali na chuma hicho, kutokana na kutoa gesi ambayo  mtu akivuta harufu yake hupiga chafya hivyo wanahofia huenda iwaka ni sumu.
“Hiki chuma, kinatoa moshi kama harufu ya gesi,  ambayo mtu akivuta tu anapiga chafya, harufu hiyo ni mbaya, tunahofia huenda ikawa ni sumu hivyo tunawashauri wananchi kutokisogelea”alisema Bw. Kanyau.
Hata hivyo, Mkuu huyo amewataka wananchi wa wilayani humo kutokuwa na wasi wasi kutokana na tayari wataalamu wa kutegua mabomu kutoka Jeshi la wananchi Tanzania (JWTZ tayari wameshafika katikaeneo la tukio kuchunguza tukio hilo.
Akizungumzia juu ya kuwepo kwa taarifa zilizogaa mkoani hapa kuwa chuma hicho kimekuwa kikiongezeka ukubwa kadri muda unavyokwenda hadi kufikia mfano wa kichuguu, alisema si kweli kwani awali wananchi walikuwa wakiliiona kwa mbali lakini, walipofika JWTZ na kukichukua na kuiweka sehemu peupe, hakiongezeki bali kiko hivyo hivyo.
Alisema kitu hicho kwa ndani kuna vyuma na kwa nje kuna mipira na ina nyuzi nyuzi.
Aidha kuhusiana na tuhuma kuwa bomu hilo limetokana na mapigano yanayoendelea nchini Kongo, wapiganaji hao ndiyo wamerusha kombora na kutua wilayani humo, alisema si kweli kwani hadi sasa hawajajua limetokea wapi.
“Si kweli, hadi sasa hakuna anayejua hicho chuma kilichosababisha mtikisiko mkubwa kiasi hicho, hatuwezi kusema kuwa labda limetoka Rwanda ama Burundi…. Bado uchunguzi unaendelea”alisema.
Kwa upande wa Kamanda wa polisi Mkoani Kagera , Phillip Kalangi akizungumza  na gazeti hili alikiri kuwepo kwa tukio hilo ambalo halijaleta madhara yoyote kwa wananchi lakini hadi sasa wataalam wa mabomu wa mkoani hapa hawajalitumbua ni kitu gani.
“Unajua mabomu yanajulika, kuna zaidi ya aina ya mabomu 300 na tunayajua, ukifika tu unatambua kuwa hii ni aina fulani ya bomu lakini hili, halijulikani, kwani lipo kama mfono wa tufe”alisema Kamanda Kalangi.
Alisema hadi sasa kuna mawasiliano yanafanyika kati ya JWT ya mkoani hapa na Makao makuu kwani kitu hicho kinahitaji uchunguzi wa hali ya juu”alisema.
Oktoba 31 mwaka huu watoto watano  wa kata ya  Ihanda wilayani Karagwe waliuawa kwa kulipukiwa na bomu la kutupwa kwa mkono wakati walipoliokota kama vyuma chakavu.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment