Thursday, November 1, 2012

Mamia wajitokeza kuwazika watoto wahanga wa mabomu Karagwe

  Paroko Msaidi wa wa Kanisa Katoliki Parokia ya Bugene,Padri Nicodem Byakatondaakihubiri katika misa takatifu ya kuombea wahanga wa bomu kijijini  Ihanda
 
 Na Theonestina Juma, Karagwe
MAMIA ya wakazi wa Wilaya ya Karagwe na viunga vyake wamejitokeza katika mazishi ya watoto waliouawa kwa kulipukiwa na bomu.
Mazishi hayo yaliofanyika katika kijiji cha Ihanda yalianza na misa takatifu ya kuombea miili ya watoto wanne yaliofanyika kwa familia Frank Robert iliopoteza watoto wanne. 
Misa hiyo ilioendeshwa na Askofu wa kanisa Katoliki Jimbo la Kayanga,Mhashamu Almachius Rwenyongeza.
Akihubiri katika misa hiyo ya mazishi, paroko Msaidi wa parokia ya Bugene,Padri Nicodem Byakatonda alisema kifo hicho kimekuja kwa ghafla wakati taifa likishudia matukio mbali mbali yanayotishia amani ya wananchi.
Alisema kifo hicho kimetokea kwa watoto wadogo ambao walipenda dini na kwamba alikuwa akishirikiana nao katika shughuli za kanisa bila kudai chochote kama malipo yao.
"Watoto hawa walipenda dini, kila nilipoenda nao vigangoni, niliambatana nao na kuwarudisha hapa nyumbani kwao bila kuniomba kitu chochote kama malipo ya ujira wao"alisema.
Hata hivyo mahubiri ya padri huyo yaliochoma mioyo ya mamia ya waombolezaji waliofurika hapo pale alipoanza kugusia kifo kilivyowapata wakiwa katika harakati za kutafuta riziki, waombolezaji hao walionesha kuhuzunika na wengine wakibubujikwa na machozi.
Alisema kutokana na kifo hicho kuwakuta watoto hao wakiwa katika harakati zao za kusaka riziki,ni wajibu sasa wazazi kufuatilia nyendo na shughuli wanazofanya watoto wao na kuwarudi.
Alisema ikizingatiwa kuwa miongoni mwao watoto hao wamo waliohitimu elimu ya msingi mwaka huu,lakini umri wao pia ni wa kutaka kudadisi mambo hivyo hata chuma walichookota walidhani kuwa huenda kingewasaidia kupata riziki walichokitegemea.
"Hiki chuma ambacho walikiokota hawa watoto,walidhani kingewasaidia, lakini wameambulia mauti, na si bure huenda chuma hicho kilitupwa na watu wasiotutakia mema, hivyo ni lazima kuishi kwa kujichunga, tusiwe wepesi wa kuokota vitu na kuvitumia ambavyo hatuvijui"alisema.
Alisema kifo hicho kinawapatia fundisho la kila mmoja kuwa makini na watu anaoishi nao, anaoshirikiana nao katika maeneo ya sherehe, vijiweni pamoja na wageni.
Katika mazishi hayo ya watoto wanne yalihudhuriwa na Mkuu wa mkoa Kagera Kanali Fabian Massawe,
ambapo majeneza hayo hayakuweza kufunuliwa kwa ajili ya watu salaam za mwisho zaidi ya watu kupita kuangalia majeneza tu kutokana na kuharibika vibaya, ambapo hata waliofuata miili yao hospitalini ni wale waliowafahamu zaidi.
Watoto waliozikwa leo ni pamoja na Fenius Frank miaka 3 na nusu, Faraja Frank Mwaka mmoja, Scatus Kamali (15) na Nelson Alfons (14).

No comments:

Post a Comment