Monday, November 26, 2012

Manispaa nipeni mkataba wa ujenzi wa soko nisome nielewe-Kagasheki

Na Theonestina Juma, Bukoba
MBUNGE wa Jimbo la Bukoba mjini, Balozi Khamis Kagasheki ameutaka uongozi wa Manispaa  ya Bukoba kutoa na kuweka wazi mkataba wa ujenzi wa soko kuu la Bukoba unaotarajia kugharimu jumla ya sh. bilioni 12 badala ya kuwa ya siri
Balozi Kagasheki ambaye pia ni Waziri wa Maliasili na Utalii, alisema hayo jana katika mkutano wake wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa  Mayunga mjini hapa.
“Mimi sijauona hata mkataba wa ujenzi wa soko kuu, nimeomba  niuone , ili nijiridhishe sijapewa.... nawambieni hadi leo hii  sijauona huo mkataba, hata sijui ni vitu gani vilivyomo katika mtakaba huo, kwa nini Watendaji wa Manispaa wabadilishe mktaba wa ujenzi huo kuwa wa siri”alisema.
Kutokana na hali hiyo, Balozi Kagasheki alisema soko hilo halitavunjwa januari 15, mwakani kama ambayo uongozi wa Manispaa ulivyopanga.
Alisema si kwamba anapinga maendeleo, lakini anachokipigania ni kutaka kujua mkataba uko vipi, isije ikafikia hatua serikali inakaanza kushtumia na vyama vya upinzani kuwa walisaini mktaba mbovu.
“Kumbukeni nchi yetu inazidi kuwa masknini kutokana na mikataba mibovu inayowekwa na baadhi ya watendaji wetu, kwa Jimbo la Bukoba sitaruhusu jambo kama hilo, mpaka nijirisheni na mkataba uliopo nijue fedha zitakazotumika katika ujenzi huo nani atawajibika kuzilipa”alisema
Na kuongeza”nipeni mkataba nisome nielewe, fedha hizo bilioni 12 zitatoka wapi, nani atazilipa, haziewezi kutoka hivi hivi wakati Manispaa iko hoi katika suala la maendeleo”
Alisema pamoja na kwamba yeye ndiye aliahidi kuleta mabadiliko ya mandhari ya Bukoba lakini si kwa mfumo wa mkataba kutowekwa wazi.
Alisema cha kushangaza katika mradi huo ni kutofanywa kwa utafiti wa Geological Technical survey  kama eneo hilo kuna maji kiasi gani isije ikafikia hatua ya  kuanza ujenzi wake wake na ukabainika kuwa kuna maji mengi na fedha zingine zaidi zitahitajika.
Nilipohoji juzi ndani ya Baraza la madiwani kama kuna utafiti wa ‘Geotec’   ulifanywa hapo kabla nilijibiwa kuwa bado wanatarajia kufanya jamani na hili nisihoji kama Mbunge”alisema
Kutokana na hali hiyo, Mbunge huyo aliushauri uongozi wa Manispaa ya Bukoba ili kurejesha imani kwa wananchi,waelekeze nguvu zake katika ujenzi wa kituo kipya cha mabasi katika kata ya Nyanga, badala ya kuburuza wananchi.
Aidha alisema kutokana na kwa sasa kuna kesi mahakamani ya kupinga kuhamishwa kwa wafanyabiashara ndani ya soko hilo wavute subira wakisubiri maamuzi ya mahakama ambayo yanatarajiwa kutolewa mwezi Machi mwakani.
Alisema wao viongozi pamoja na watendaji wa Manispaa ya Bukoba wanatakiwa kufanya kazi kama timu moja kwani hakuna kitakachowashinda na  wasitishane kwa vitu vidogo.
Alisema lengo lao wote kwa pamoja ni kulinda maslahi ya mtu wa kawaida aliyewapa nafasi ya uongozi  na wasiende kibabe.
Mwisho.

Bomu lazua tafrani Ngara

Na Theonestina Juma, Bukoba
WANANCHI  wanaoishi karibu na uwanja wa ndege katika  kijiji cha  Ruganzo kata ya Kibimba wilayani Ngara wamegubikwa na hofu kubwa baada ya kitu kizito mithili ya bomu inayotoa hewa ya gesi  ambayomtu akivuta anapiga chafya kudondoka chini kwa kishindo kutoka juu na kusababisha milipuko mingi kutokea.
Tukio hilo la aina yake na ya mara ya kwanza kutokea wilayani humo ambalo linapakana na nchi zaidi ya nne za Afrika Mashariki lilitokea Novemba 22 mwaka huu saa 8 usiku wakati wananchi wakiwa wamelala.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Mkuu wa wilaya ya Ngara, Costantine Kanyasu alisema kitu hicho mfano wa chuma lenye umbo kama la yai  linalotoa hewa ya gesi lilipodondoka chini kwa nguvu na kusababisha  mtikisiko mkubwa wilayani humo jambo lililochangia wananchi kujawa na hofu kubwa.
Alisema pamoja na kutokea milipuko zaidi ya mara tatu wilayani humo haijajulikana kama yamesababishwa na kudondoka kwa chuma hicho ambacho hadi sasa hakijathibitishwa kama ni bomu.
Alisemakutokana na kuwepo sintofahamu kwa wananchi wanaoishi karibu na eneo hilo la uwanja wa ndege, kamati ya ulinzi na usalama umewashauri wananchi kukaa mbali na chuma hicho, kutokana na kutoa gesi ambayo  mtu akivuta harufu yake hupiga chafya hivyo wanahofia huenda iwaka ni sumu.
“Hiki chuma, kinatoa moshi kama harufu ya gesi,  ambayo mtu akivuta tu anapiga chafya, harufu hiyo ni mbaya, tunahofia huenda ikawa ni sumu hivyo tunawashauri wananchi kutokisogelea”alisema Bw. Kanyau.
Hata hivyo, Mkuu huyo amewataka wananchi wa wilayani humo kutokuwa na wasi wasi kutokana na tayari wataalamu wa kutegua mabomu kutoka Jeshi la wananchi Tanzania (JWTZ tayari wameshafika katikaeneo la tukio kuchunguza tukio hilo.
Akizungumzia juu ya kuwepo kwa taarifa zilizogaa mkoani hapa kuwa chuma hicho kimekuwa kikiongezeka ukubwa kadri muda unavyokwenda hadi kufikia mfano wa kichuguu, alisema si kweli kwani awali wananchi walikuwa wakiliiona kwa mbali lakini, walipofika JWTZ na kukichukua na kuiweka sehemu peupe, hakiongezeki bali kiko hivyo hivyo.
Alisema kitu hicho kwa ndani kuna vyuma na kwa nje kuna mipira na ina nyuzi nyuzi.
Aidha kuhusiana na tuhuma kuwa bomu hilo limetokana na mapigano yanayoendelea nchini Kongo, wapiganaji hao ndiyo wamerusha kombora na kutua wilayani humo, alisema si kweli kwani hadi sasa hawajajua limetokea wapi.
“Si kweli, hadi sasa hakuna anayejua hicho chuma kilichosababisha mtikisiko mkubwa kiasi hicho, hatuwezi kusema kuwa labda limetoka Rwanda ama Burundi…. Bado uchunguzi unaendelea”alisema.
Kwa upande wa Kamanda wa polisi Mkoani Kagera , Phillip Kalangi akizungumza  na gazeti hili alikiri kuwepo kwa tukio hilo ambalo halijaleta madhara yoyote kwa wananchi lakini hadi sasa wataalam wa mabomu wa mkoani hapa hawajalitumbua ni kitu gani.
“Unajua mabomu yanajulika, kuna zaidi ya aina ya mabomu 300 na tunayajua, ukifika tu unatambua kuwa hii ni aina fulani ya bomu lakini hili, halijulikani, kwani lipo kama mfono wa tufe”alisema Kamanda Kalangi.
Alisema hadi sasa kuna mawasiliano yanafanyika kati ya JWT ya mkoani hapa na Makao makuu kwani kitu hicho kinahitaji uchunguzi wa hali ya juu”alisema.
Oktoba 31 mwaka huu watoto watano  wa kata ya  Ihanda wilayani Karagwe waliuawa kwa kulipukiwa na bomu la kutupwa kwa mkono wakati walipoliokota kama vyuma chakavu.
Mwisho.

Tuesday, November 20, 2012

Mwanamke amuua mwanae kwa kumtwanga kichwani na kisha kumzika chap chap


BUKOBA
JESHI la polisi Mkoani Kagera linamshikilia  Bi. Johnmary Anthony kwa tuhuma ya kumuua mwanae wa miezi mitatu kwa kumtwanga na kitu kizito kichwani na kufariki papo hapo na kisha kumfukia chap chap kwenye shimo la kutupia takataka akiwa  amemfunga kwenye  mifuko ya plastic maarufu kama kiroba
Kwa mujibu wa habari zilizopatikana mjini hapa na kuthibitishwa na Kamanda wa polisi Mkoani hapa, Phillip Kalangi tukio hilo la aina yake  na la kusikitisha limetokea Novemba 16 mwaka huu katika kijiji cha Kyaitoke Bukoba vijijijini.
 Kifo cha mtoto huyo kiligunduliwa na uongozi wa kijiji hicho, baada ya mtoto huyo kupita takribani siku nzima haonekani kama mama yake amembeba wala kumnyonyesha kama ilivyozoeleka jambo lililolazimu uongozi wa kijiji hicho kutoa taarifa katika kituo cha polisi.
Mwanamke huyo inadaiwa kuwa alihojiwa na uongozi wa kijiji hicho aliko mtoto ambapo alikuwa akiwadanganya kuwa mtoto amepotea jambo lililowatia hofu na kuamua kutoa taarifa kituo cha polisi .
Kutokana na hali hiyo, mwanamke huyo akihojiwa na polisi alidai kuwa hajui mtoto alipo, hali lililolazimu jeshi hilo kuzidi kumhoji kwa makini ambapo alisema kuwa mtoto huyo amemuua kwa kumpiga na kitu kizito kichwani.
 Kamanda Kalangi alisema pamoja na kuendelea kuhojiwa kwa mwanamke huyo, hajakubali kumtaja hata jina la mtoto huyo, wala hata sababu iliompelekea kumuua mwane kwa kumtwanga kichwani na kitu kizito.
Kamanda huyo alisema mwanamke huyo bado anaendelea kuhojiwa, ambapo anatajiwa kupimwa akili kwanza ili kuangalia kama ni mgonjwa wa akili kabla ya kupandishwa kizimbani.
mwisho

Saturday, November 17, 2012

Wananchi muda wa kufungwa viongozi wetu pingu na kuletwa mbele yetu ni enzi za wakoloni


Na Theonestina Juma, MISSENYI
KITENDO cha Jeshi la polisi Wilayani Missenyi, kumfunga pingu Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mutukula, Bw.Hamidu Mugarula na kuanza kumzungusha mtaa mzima kwa  ajili ya kumtaka awaoneshe wananchi aliowauzia maeneo kwa ajili ya kufanyiabiashara kimezua mapambano makubwa kati ya polisi na wananchi hadi kusababisha polisi kupiga risasi kadhaa hewani na mabomu la machozi
Tukio hilo la aina yake lililoonekana kama sinema na kuwalazimu baadhi a wanachi kukimbia upande wa Uganda kujiokoa kilitokea hivi karibuni (Novemba 6) mwaka huu saa 8 mchana katika eneo la Mutukula mpakani mwa Tanzania na Uganda.
Mapambano hayo yaliodumu kwa saa 5 ililazimu polisi wengine  kuitwa kutoka mjini Bukoba, kwenda kuongeza nguvu ambapo muda huo wote shughuli za biashara na usafirishaji katika eneo hilo la mpakani zilisimama.
Wakizungumza  na gazeti hili,  baadhi ya wananchi na wafanyabishara walioshuhudia tukio hilo walisema chanzo cha mapambano hayo kati ya polisi na wananchi ni baada ya wananchi kuchukizwa na kitendo cha kiongozi wao akiwa amefungwa pingu huku akiwa ametangulizwa mbele na polisi akizungushwa mtaa mzima wakimtaka awaoneshe watu aliowakatia risiti za kuuziwa maeneo kwa ajili ya kufanyia biashara.
Walisema kutokana na hali hiyo, kuliibuka mzozo mkubwa kati ya polisi na wananchi hao, ambao waliwasihi polisi kumfungua pingu kiongozi wao kama wanataka waongee nao.
Alisema wananchi hao walidai kuwa kiongozi wao hawezi kuletwa mbele yao akiwa amefungwa pingu kama mwizi wakati alikuwa akifanya kazi za serikali.
Kutokana na hali hiyo, huku jeshi la polisi, wakiwa hawaelewani na wananchi hao, kwa hasira walianza kufanya vurugu ikiwa ni pamoja na kuwarushia mawe polisi waliokuwa na mwenyekiti huyo, ambapo polisi walipoona hali ni mbaya walilazimika kumbeba mwenyekiti huyo kama ng’ombe na kumtumbukiza ndani ya gari waliokuwa nao na kumkimbiza katika kituo cha polisi cha Kyaka.
Hata hivyo, kitendo hicho kinaelezwa kuwa kilionesha kuzidi kuwakasirisha wananchi hao, na kuamua kukimbia kwenda kufunga kizuizi na kuanza kupanga matairi kwa lengo la kutaka kuharibu gari la polisi ili kumtoa kiongozi wao.
Polisi waliwawahi kupita eneo hilo, ambapo baada ya kuona polisi hao wameondoka na kiongozi huyo, walihamishia hasira zao  kwenye mali za serikali .
Wananchi hao  walivamia ofisi ya kijiji cha Mutukula na kung’oa mlango na madirisha  na kuchoma moto bendera ya Chama cha mapinduzi (CCM) kilichokuwa kikipepea maeneo hayo na kisha kuhamia katika jengo lililokuwa likitumia na halmashauri ya missenyi kwa ajili ya kukatia ushuru na kuliteketeza kwa moto pamoja na nyaraka zote zilizokuwemo.
Mwenekiti wa Katibu wa soko na wafanyabiashara katika eneo hilo la Mutukula, Bw. Theophil Kaembe akizungumza na gazeti hili alisema  katika eneo la Mutukula, kuna eneo lililotengwa na serikali kwa ajili wa ujenzi wa kituo cha mabasi ambapo eneo hilo kutokana na kukaa wazi muda mrefu, huku wananchi wakihangaikia  kutafuta sehemu pa kufanyia biashara,mwenyekiti huyo kwa kushirikiana na Mtendaji wa Kata, Bw.Mukasa Mugarula waliamua kuwagawawia wananchi hao.
Alisema maeneo hayo waligawa kwa kulipia sh. 10,000 ambapo walielezwa kuwa maeneo hayo wamegawawiwa kwa muda kutokana na eneo hilo  ni la serikali na linaweza  kuhitajiwa kwa matumizi aliolengwa kwa muda wowote.
Bw. Kaembe alisema “hata risiti tulizokatiwa zimeandikwa kuwa ni kwa muda si za kudumu, risiti walizozitumia ni ya halmashauri namba HW5”.
Mapambano hao ambayo ililazimika polisi kutolewaa mjini Bukoba kwenda kuongeza nguvu kutuliza ghasia hizo, ilivutia hisia za viongozi, wa mkoani hapa, ilimlazimu hadi Kamanda wa polisi Mkoani hapa, Phillip Kalangi na Mkuu wa wilaya hio, Issa Njiku kufika eneo hilo.
Hata hivyo, Kamanda Kalangi akizungumzia vurugu hizo, alisema kuwa imetokana na malalamiko yaliotolewa na baadhi ya wananchi kuwa wanatakiwa warudishe maeneo hayo wakati waliuziwa kati ya sh. 200,000 hadi 350,000.
Alisema pamoja na vurugu hizo kutokea na kusababiasha shughuli nyingi za kibiashara kusimama kwa muda lakini tayari walishafanya mazungumzo na wananchi wa maeneo hayo na nchi jirani na kusawazisha na hivyo hali imerudi ya kawaida.
Alisema viongozi hao wanaoshikiliwa na jeshi hilo wanatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote, kwa tuhuma a kutumia ofisi ya na wameuziwa maeneo na viongozi wa serikali kutumia vibaya ofisi ya serikali.
mwisho

Thursday, November 15, 2012

Majambazi wateka Muleba, wampora mfanyabiashara milioni 60 na kumuua mulinzi

Na Theonestina Juma, Muleba
MAJAMBAZI wenye silaha wamemuua, mlinzi wa kituo cha mafuta cha JR Petrol Bw.Felix Tonswe (55) ameuawa na majambazi waliofika kituoni hapo kumfuatilia mfanyabiashara mmoja wa duka wa Nshamba kwa lengo la kumpora fedha milioni 60 alizokuwa nazo.
Tukio hilo lilitokea Novemba 12, mwaka huu  majira ya mchana wakati mfanyabiashara kutoka Nshamba aliyejulikana  ka jina la Cleophace Rweyemamu (32) aliyekuwa safarini kuelekea Jijini Mwanza kulangua bidhaa.
Habari hizo zinasema kuwa, watu sita waliodhaniwa kuwa ni majambazi wakiwa na silaha, walianza kumfuatilia mfanyabiashara huyo kutoka Nashamba wakiwa na pikipiki tatu walizokuwa wamepakiana wawili wawili kama abiria.
Majamjazi hayo walikuwa akifuatilia nyendo za mfanyabiashara huyo bila kujua, ambapo alipofika katika kituo cha mafuta kwa jili ya kuwekewa mafuta kwenye gari lake, majambazi hayo sita waliingia kituoni hapo na kukizingira ambapo walimwamuru mfanyabiashara huyo kulala chini kifudi fudi.
Kutokana na mfanyabiashara huyo kutii  agizo la majambazi hayo, walimpora sanduku lake lililokuwa na jumla ya sh. milioni 60 na kumwacha bila kumdhuru.
Hata hivyo katika harakati hizo, mlinzi wa kituo hicho alianza kujihami nao kwa kutumia silaha yake aliokuwa nayo lakini majambazi hayo walimuwahi na kumpiga risasi sehemu za matakoni ambapo alianguka  chini  na kupoteza fahamu.
  Tukio hilo ambalo limethibitishwa na Kamanda wa polisi Mkoani Kagera, Phillip Kalangi , alisema watu watatu wanashikiliwa na jeshi hilo kuhusika na tukio hilo ambapo msako bado unaendelea wa kuwatafuta watu wengine waliohusika katika uporaji na mauji hayo.
Katika tukio hilo Kamanda Kalangi alisema inasadikika kuwa aina ya bunduki iliotumiwa na jambazi hayo ni kati ya SMG au ASR kutokana na risasi zilizotumika.
Hata hivyo, kamanda huyo ametoa tahadhari kwa wafanyabiashara mkoani hapa kuacha kutembea na kiasi kikubwa cha fedha wakati ambapo mfumo wa utunzaji wa fedha umeboreshwa hapa nchini.

Wavuvi saba wafa maji Ziwa Victoria

Na Theonestina Juma, Bukoba
WAVUVI saba katika Ziwa Victoria wakati wakitoka kuvua samaki katika eneo la hifadhi serikali la Rubundo katika kisiwa cha Ikuza wlayani Muleba Mkoani Kagera.
  wamefariki dunia katika matukio mawili tofauti  wilayani Muleba Mkoani Kagera likiwemo la wavuvi saba kufa maji katika ziwa Victoria wakati wakitoka kuvua samaki na mtu mmoja kuuawa na majambazi.
Kwa mujibu wa habari zilizopatikana kutoka wilayani Muleba  tukio la kwanza la wavuvi kufa maji lilitokea Novemba 10, mwaka huu saa 9 usiku katika eneo la hifadhi ya Rubondo na Kambi ya wavuvi ya Kaziramtemwa katika kisiwa cha Ikuza wilayani humo.
Wavuvi hao walikufa maji wanadaiwa kuwa walikuwa ni wavuvi haramu, ambao walienda kuvua samaki katika hifadhi ya akiba ya Rubondo ambalo limetengwa rasmi na serikali kwa ajili ya mazalia ya samaki.
Imeelezwa kuwa chanzo cha wavuvi hao kufa maji ndani ya ziwa Victoria, ni kutokana na mtumbwi waliokuwa nao  ulielemewa na mzigo mkubwa wa samaki waliokuwa wamevua katika eneo hilo la hifadhi.
Kwa mujibu wa vyanzo vya uhakika wa habari hizi, wavuvi hao wakati wakienda kuvua samaki katika eneo hilo hawakuwenda na mtumbwi wa mashine bali la makasia, ambapo wakati wakirejea mtumbwi huo ulielemewa na mzigo na hivyo maji yalikuwa yalikuwa  ndani ya mtumbwi huo ambao ulisababisha kupinduka na kuzama.
Katika mtumbwi huo uliokuwa na jumla ya watu tisa wavuvi saba walifariki na wengine wawili waliokoka baada ya kuogelea hadi nchi kavu.
Wavuvi waliokufa maji wametambuliwa kuwa ni pamoja na Baluya Masala (28), Obeid Yohana (33), Juma Kengele (35) wote wakazi Muganza wilayani Chato mkoani Geita.
Wengine ni pamoja na Alex Mwita (40) mkazi wa wilayani Tarime na Kipara Kasukari (40) mkazi wa wilayani Muleba.
Wengine waliotambuliwa kwa jina moja moja ni pamoja na Nicko  (33) mkazi wa wilayani Sengerema Jijini Mwanza na Robert  (32) mkazi wa Wilayani Biharamulo mkoani Kagera na kwamba kati ya watu hao wanne wamesafirishwa na wengine wamezikwa kisiwani humo.
Aidha walionusurika katika ajali hiyo wamejulikana kuwa ni pamoja na Robert Abdul (37) mkazi wa wilayani Tarime na Khamis Musa (28) mkazi wa Muganza wilayani Chato.
wavuvi wanne tayari wameshasarishwa  na kuzikwa huku wengine watatu wakizikwa kisiwani humo.
Mwisho.

Wednesday, November 7, 2012

Barack Obama ambwaga mpinzani wake Mitt Romney

Hotuba yake ya ushindi
Rais wa Marekani Barack Obama amechaguliwa tena kwa muhula wa pili na kumshinda mpinzani wake wa Republican Mitt Romney.
Barack ambaye ni rais wa kwanza mweusi wa Marekani, alipata kura 270 za (Electral College) zilizohitajika ili kupata ushindi.
Kura hizi hupigwa na watu maalum wanaoteuliwa na majimbo kulingana na idadi ya miji katika majimbo hayo.
Katika hotuba yake ya ushindi, mbele ya umati mkubwa wa watu mjini Chicago, Obama alisema kuwa atashauriana na bwana Romney kuhusu wanavyoweza kuendesha nchi hiyo.
Aidha Obama aliweza kuwashawishi wananchi kumpigia kura na hivyo kushinda licha ya changamoto nyingi zilizowavunja moyo wananchi hususan swala la uchumi.
Obama pia alikabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa mshindani wake Mit Romney.
Wabunge wake wa Democrats waliweza kusalia na idadi yao kubwa katika bunge la Senate ambalo wameshikilia tangu mwaka 2007.
Wabunge wa Republican nao wataendelea kudhibiti bunge la waakilishi, hatua ambayo wadadisi wanasema kuwa huenda likasalia kuwa kikwazo kikubwa kwa Obama na mipango yake ya nchi hasa kuhusu maswala ya sheria.
Sherehe zilizofuata ushindi wa Barack Obama
Katika hotuba yake ya ushindi Obama aliwataka wapinzani wake kushirikiana naye kuleta mageuzi nchini humo.
Zikiwa zimesalia tu kura 29 kutoka kwa jimbo la Florida, Obama aliweza kushinda kura 303 dhidi ya kura 206 za Mit Romney.
Katika kura za ujumla zilizopigwa na wananchi ambazo ni muhimu kisiasa ingawa sizo ambazo zinampa rais ushindi , ushindani mkali ulidhirika kwani Obama alipata asilima hamsini huku Romney akipata asilimia 48.
Obama alimpongeza bwana Romney na mgombea mwenza wake Paul Ryan kwa kuendesha kampeini yao iliyokuwa na ushindani mkubwa.
Bwana Obama alisema anarejea ikulu ya White house akiwa na motisha zaidi kumaliza kazi aliyoianzisha na kuhakikisha mustakabali mwema kwa wamarekani.
Obama alituma ujumbe kwenye Twitter baada ya kupata taarifa za ushidni wake akiwashukuru wapiga kura
Katika hisia zilizotolewa kote ulimwenguni kufuatia ushindi wa rais Obama, Wizara ya mambo ya nje ya Uchina imesema rais Hu Jintao na waizri mkuu Wen Jiabao wamempongeza Obama kuchaguliwa tena kuwa rais.
Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron, amesema Rais Obama amekuwa kiongozi mwenye mafanikio na alitazamia kuendelea kufanya kazi naye.
Rais wa Umoja wa Ulaya Herman van Rompuy, amesema ana furaha kuhusu ushindi wa rais Obama. Naye waziri mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu amesema uhusiano kati ya nchi yake na Marekani umezidi kuwa na nguvu kushinda siku za nyuma.

Sunday, November 4, 2012

Miss Mara 2012 awa Miss Tanzania NA.2

MSHINDI WA REDDS MISS TANZANIA 2012 BRIGITER ALFRED
AKIVISHWA TAJI NA MSHINDI WA MISS TANZANIA 2011 SALHA ISRAEL
WAREMBO WALIO INGIA TANO BORA





MSANII RECHO AKIWA NA WACHEZAJI WAKE



VAZI LA UFUKWENI

Saturday, November 3, 2012

Bridgit ndiye miss Tanzania 2012


REDDS MISS TANZANIA 2012, BRIDGIT ALFRED (KATI) AKIWA KATIKA PICHA YA PAMOJA NA MSHINDI WA PILI EUGENE FABIAN NA MSHINDI WA TATU EDA SYLVESTA (KULIA). 

Thursday, November 1, 2012

Nishati ya mafuta ya Dizeli, Petroli yaadimika Karagwe

 Angalia mwenyewe  shida ya upatikanaji wa nishati ya mafuta Karagwe, hakuna cha foleni kila mtu kivyake ilimradi apate tu mafuta ya dizeli ama petroli
 Hiki kituo peke yake katika mji wa Kayanga ndicho kilikuwa kikijikongoja kuwa na mafuta kiduchu
 Mwanagu ehee, leta nikumiminie ili niwahi tena kutafuta mengine
 Magari lakini ni kwa foleni, bila hivyo si  ni ajali mwanangu!

Ndiyo hii ni foleni ya kusaka mafuta.

Ihanda ni vilio tu, watoto watano waliolipukiwa na bomu

 sehemu ya mamia waliojitokeza kusindikiza wahanga wa bomu safari yao ya mwisho hapa duniani

 Kila mtu alitafuta sehemu pa kujinga mvua ilimradi tu wahakikishe watoto waliowaona saa chache kulipukiwa na bomu la kutupwa kwa mkono
 Hii ni njia ya kila mmoja wetu, kwa heri watoto wetu
 Kweli ni huzuni
 Bw.Frank Robert aliyepoteza watoto watatu kwa mpigo akiwa katika huzuni
 Askofu wa kanisa Katoliki Jimbo la Kayanga akizungumza kwa huzuni katika misa ya kuwaombea safari ya mwisho watoto ambao ni wahanga wa bomu
Tunabanana humu huu mpaka tushuhudie miili ya wapendwa wetu ukishushwa katika nyumba yao ya milele

Mamia wajitokeza kuwazika watoto wahanga wa mabomu Karagwe

  Paroko Msaidi wa wa Kanisa Katoliki Parokia ya Bugene,Padri Nicodem Byakatondaakihubiri katika misa takatifu ya kuombea wahanga wa bomu kijijini  Ihanda
 
 Na Theonestina Juma, Karagwe
MAMIA ya wakazi wa Wilaya ya Karagwe na viunga vyake wamejitokeza katika mazishi ya watoto waliouawa kwa kulipukiwa na bomu.
Mazishi hayo yaliofanyika katika kijiji cha Ihanda yalianza na misa takatifu ya kuombea miili ya watoto wanne yaliofanyika kwa familia Frank Robert iliopoteza watoto wanne. 
Misa hiyo ilioendeshwa na Askofu wa kanisa Katoliki Jimbo la Kayanga,Mhashamu Almachius Rwenyongeza.
Akihubiri katika misa hiyo ya mazishi, paroko Msaidi wa parokia ya Bugene,Padri Nicodem Byakatonda alisema kifo hicho kimekuja kwa ghafla wakati taifa likishudia matukio mbali mbali yanayotishia amani ya wananchi.
Alisema kifo hicho kimetokea kwa watoto wadogo ambao walipenda dini na kwamba alikuwa akishirikiana nao katika shughuli za kanisa bila kudai chochote kama malipo yao.
"Watoto hawa walipenda dini, kila nilipoenda nao vigangoni, niliambatana nao na kuwarudisha hapa nyumbani kwao bila kuniomba kitu chochote kama malipo ya ujira wao"alisema.
Hata hivyo mahubiri ya padri huyo yaliochoma mioyo ya mamia ya waombolezaji waliofurika hapo pale alipoanza kugusia kifo kilivyowapata wakiwa katika harakati za kutafuta riziki, waombolezaji hao walionesha kuhuzunika na wengine wakibubujikwa na machozi.
Alisema kutokana na kifo hicho kuwakuta watoto hao wakiwa katika harakati zao za kusaka riziki,ni wajibu sasa wazazi kufuatilia nyendo na shughuli wanazofanya watoto wao na kuwarudi.
Alisema ikizingatiwa kuwa miongoni mwao watoto hao wamo waliohitimu elimu ya msingi mwaka huu,lakini umri wao pia ni wa kutaka kudadisi mambo hivyo hata chuma walichookota walidhani kuwa huenda kingewasaidia kupata riziki walichokitegemea.
"Hiki chuma ambacho walikiokota hawa watoto,walidhani kingewasaidia, lakini wameambulia mauti, na si bure huenda chuma hicho kilitupwa na watu wasiotutakia mema, hivyo ni lazima kuishi kwa kujichunga, tusiwe wepesi wa kuokota vitu na kuvitumia ambavyo hatuvijui"alisema.
Alisema kifo hicho kinawapatia fundisho la kila mmoja kuwa makini na watu anaoishi nao, anaoshirikiana nao katika maeneo ya sherehe, vijiweni pamoja na wageni.
Katika mazishi hayo ya watoto wanne yalihudhuriwa na Mkuu wa mkoa Kagera Kanali Fabian Massawe,
ambapo majeneza hayo hayakuweza kufunuliwa kwa ajili ya watu salaam za mwisho zaidi ya watu kupita kuangalia majeneza tu kutokana na kuharibika vibaya, ambapo hata waliofuata miili yao hospitalini ni wale waliowafahamu zaidi.
Watoto waliozikwa leo ni pamoja na Fenius Frank miaka 3 na nusu, Faraja Frank Mwaka mmoja, Scatus Kamali (15) na Nelson Alfons (14).

Hivi ndivyo hali halisi ilivyokuwa katika mazishi ya watoto wanne wa familia moja waliolipukiwa na bomu

 Mzazi wa mhanga wa bomu wilayani Karagwe, mzee Kamali akizungumza wakati wa misa ya kuombea miili ya marehemu kabla ya kuzikwa.

 Baadhi ya waombolezaji wakiwa wanasikitika mbele ya jeneza la mtoto Scatus Kamali
 Mama mzazi huyo aliyeinama kwa majonzi aliyepoteza watoto watatu kwa mpigo katika ajali ya bomu, akilia kwa uchungu wakati akitoa salaam za mwisho katika majeneza ya watoto wake.
 Majeneza yaliobeba miili ya watoto wanne wa familia moja yakiwa yanaombea tayari kwa maziko