Monday, April 7, 2014

Polisi wa Uganda wazua tafrani mpakani mwa Tanzania na Uganda, waingia nchini kinguvu wananchi wampora mmoja wao silaha ,RPC agoma kuzungumzia

Na Theonestina Juma, Bukoba KATIKA hali isiyo ya kawaida, polisi wanne wenye silaha kutoka nchini Uganda wameingia nchiniTanzania upande wa Mutukula kinguvu na kuanza kurusha risasi ovyo na kuwajeruhi watu wawili. Akizungumza na blog hii njia ya simu, Mkuu wa wilaya ya Missenyi, Kanali Issa Njiku alisema tukio hilo la aina yake lilitokea Aprili 6, mwaka huu saa 11.30 jioni. Alisema wananchi wawili waliojeruhiwa katika tukio hilo la polisi wa nchini Uganda kurusha risasi ovyo mmoja ni raia wa Tanzania ambaye ni mtu mzima na mwingine ni mtoto raia wa nchini Uganda. Kanali Njiku alisema chanzo cha polisi hao kuingia nchini kwa nguvu ni kutokana na kile kinachoelezwa na wao kuwa walikuwa katika msako wa kukamata pikipiki za wizi Mbarambara nchini mwao. Alisema katika harakati hizo, walimkamata mwizi mmoja aliyeiba pikipiki ambapo katika mahojiano yao alikiri kuiba na kwamba pikipiki hiyo ameiuza nchini Tanzania upande wa Mtukula. “Naweza kusema kuwa ni katika hali ya polisi kujitafutia tu riziki, polisi hao wanasema kuwa walikuwa wamemkata mwizi aliyewataka waje Tanzania akawaoneshe mtu aliyemuuzia pikipi alioiba, walifanya hivyo bila kufuata utaratibu wan chi husika”alisema. Alisema polisi hao walipofika katika kuzuizi cha mpaka wa Tanzania na Uganda, walianza kufyatua risasi ovyo, jambo lililowalazimua wananchi upande wa Tanzania kuwavamia kwa lengo la kutaka kuwanyang’anya silaha. “Katika tukio hilo, ilikuwa ni purukushani, wananchi waliwavamia polisi hao waliokuwa wakirusha risasi kwa lengo la kuwanyang’anya silaha ambapo walifanikiwa kumkamata polisi mmoja lengo ilikuwa kuwadhibiti wasiendelee kurusha risasi ndipo risasi ziliwapata watu hao na kuwajeruhi”. Hata hivyo, alisema polisi watatu walifanikiwa kuwatoroka wananchi hao pamoja na silaha zao na mmoja ndiye walifanikiwa kumkamata ambapo hawakuweza kumdhuru. Alisema Polisi wa Uganda waliohusika katika tukio hilo, si wale wanaoishi maeneo ya mpakani hapo, bali ni kutoka Mbarambara. Alisema Mtanzania alijeruhiwa mkono wake wa kushoto na Mganda ambaye ni mtoto amejeruhiwa mguu wa kushoto ambapo wote wamelazwa katika kituo cha afya cha Bunazi na hali zao zinaendelea vizuri. Alisema kutokana na tukio hilo, taari kamati ya ulinzi na usalama kutoka wilaya jirani zote zinazopakana zilikaa jana usiku kujadili suala hilo ambapo polisi waliohusika wamekamatwa. Aidha kwa sasa kikao cha kamati ya ulinzi na usalama wa mkoa unaosubiriwa kukaa kujadili suala hilo. Kwa upande wa Kamanda wa Polisi Mkoa Kagera, George Mayunga alipoulizwa na gazeti hili kuhusu tukio hilo, alikiri kutokea na kusema kuwa hawezi kulizungumzia kwa vile linashughulikiwa na vyombo vya juu. “Suala la Mutukula siwezi kulizunguzia kwa sasa, muda wake muafaka utakapofika nitalizungumzia, lakini kwa leo hapana linashughulikiwa na ngazi za juu’alisema. Kutokana na hali hiyo Kamanda huyo hakuwa tayari kutaja hata majina ya majeruhi wa tukio hilo. Kwa utaratibu, kama nchi jirani inamtafuta mhalifu anapaswa kufuata utaratibu wa kuwasiliana na polisi wa nchi husika kufanya upelelezi wake na kumkata mtuhumiwa huyo na si polisi kutoka nchi nyingine kuingia kinguvu katika nchi husika bila taarifa. Mwisho.

No comments:

Post a Comment