Dar es Salaam. Maandalizi ya ujio wa Rais wa
Marekani, Barack Obama nchini yanazidi kupamba moto huku maofisa wa
usalama wa Marekani wakipiga kambi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa
wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam.
Aidha, kutokana na ujio huo, Serikali imeagiza
mashirika yote ya ndege kubadili ratiba zao za safari Julai Mosi, siku
ambayo Rais huyo atatua nchini.
Jana, waandishi wetu walishuhudia pilikapilika za
kuimarisha ulinzi katika uwanja huo jambo ambalo uongozi wa uwanja huo
jambo wamelieleza kwamba halijawahi kutokea.
Ulinzi haujawahi kutokea
Mkurugenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Julius Nyerere, Moses Malaki alisema jana kwamba ratiba za uwanjani hapo
zitabadilika kutokana na uzito wa ugeni huo.
Alisema kwa kawaida anapokuja kiongozi mkubwa wa
kitaifa katika uwanja huo hakuna ndege inayoruhusiwa kutua kwa kipindi
cha nusu saa.
“Ni kweli hali hiyo pia itakuwapo atakapokuja Rais
Obama na safari za ndege zitabadilika kulingana na ratiba ya kutua na
kuondoka kwa Rais huyo,” alisema Malaki.
Pia alisema ulinzi katika uwanja huo umeimarishwa
kwa mwezi mmoja sasa na tangu wakati huo, maofisa wa usalama wa Marekani
wamekuwa wakifika kwa nyakati mbalimbali.
“Sijawahi kuona ulinzi mkali kama huu, wamekuja
marais wengi hapa nchini lakini ulinzi huu ni wa kutisha, sijui kwa
sababu gani?” alisema Malaki.
Alisema awali, wakati maofisa hao walipoanza
kuwasili nchini hawakutambua ni mgeni gani anayetarajia kufika lakini
baadaye walipelekewa taarifa kuwa ni Rais Obama na baadaye walitaarifiwa
kuwa angetua saa 8.40 mchana, Julai Mosi.
Mkurugenzi huyo alisema Rais Obama atakuja na
ndege nne, moja itakayombeba, ya pili kwa ajili ya mizigo, ya tatu
itakuwa ya waandishi wa habari na maofisa wa usalama na ya mwisho ni kwa
ajili ya dharura ambayo itaegeshwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa
wa Kilimanjaro (KIA).
Malaki alisema maofisa wa Marekani wanaowasili
nchini wamekuwa wakifanya shughuli mbalimbali za kuhakikisha kuwa hali
ya usalama inaimarishwa na kuwaacha wazawa wakifanya shughuli za
kawaida.
No comments:
Post a Comment