Mwanamama akipita katika ukuta wenye
picha ya Nelson Mandela mjini Soweto. Mandela anapatiwa matibabu huko Pretoria
na hali yake inaelezwa kuwa ni mahututi na wananchi wamekuwa wakimwombea nafuu
ya haraka. Picha ya AFP
Habari zilizotapakaa katika maeneo mbalimbali ya Jiji la
Johannesburg ni kwamba hakuna matumaini ya Mandela kupona na sasa familia yake
inajadiliana kuhusu taratibu za mazishi yake huku mwenyewe akiendelea kupumua
kwa msaada mashine hospitalini alikolazwa.
Mandela (94) amelazwa katika
Hospitali ya Magonjwa ya Moyo, Med – Clinic, Pretoria kwa siku ya 19 sasa na
taarifa ambazo zimekuwa zikitolewa na Ikulu ya Afrika Kusini tangu Jumapili,
usiku zinathibitisha kwamba hali yake ni mahututi.
“Tunasubiri habari mbaya za kifo cha
Mandela maana taarifa zinazotolewa na Serikali kuhusu hali ya afya yake ni
dalili kwamba hawezi kuishi tena,” alisema mkazi wa Johannesburg, Doroth Nyathi
alipozungumza na mwandishi wetu na kuongeza:
“Watu wanaamini kwamba Mandela
ameshafariki dunia, lakini Serikali na familia yake wanatuficha tu, labda
wanasubiri maadhimisho ya siku yake ya kuzaliwa mwezi ujao.”
Mandela anafikisha umri wa miaka 95
Julai 18 mwaka huu, lakini kuna wasiwasi kwamba huenda asiifikie siku hiyo
ambayo ni maarufu kama “Mandela Day” kutokana na kuzorota kwa afya yake.
“Kama mtu hajafa mnawezaje kukaa
kujadili mahali pa kumzika, ndiyo maana nimekwambia ni dhahiri kwamba Mzee
Madiba (Mandela) tayari amefariki, ila wanatuficha tu,” alisema Nyathi.
Nyathi alikuwa akirejea taarifa za
vyombo vya habari kwamba familia ya Mzee Mandela ilikutana katika kikao cha
siri juzi kati ya saa 5:00 asubuhi na saa 08:00 mchana kujadili “mahali pa
maziko” ya shujaa huyo aliyeongoza mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi,
kufungwa jela miaka 27 na baadaye kuwa Rais wa kwanza mzalendo wa Afrika
Kusini.
Habari kutoka katika kikao hicho
kilichohudhuriwa na waziri katika Serikali ya Afrika Kusini ambaye pia ni
mwanafamilia wa Mandela na mmoja wa viongozi wa vyama vya siasa, zinasema
baadhi walikuwa wakitaka azikwe alikozaliwa huko Mvezo, wakati wengine wakitaka
azikwe Qunu.
Baadhi ya vyombo vya habari vya
Afrika Kusini vimesema Mandela atazikwa Qunu, taarifa ambazo hata hivyo,
hazijathibitishwa na Serikali ya Afrika Kusini ambayo imekuwa ikisisitiza
kwamba “Familia ya Mandela isaidiwe katika kipindi hiki kigumu.”
Kwa upande wake, mkazi wa Pretoria,
Lisa Wright alisema wasingependa kumpoteza Mandela lakini kwa jinsi hali
inavyoendelea ni dhahiri kwamba maradhi yanamzidi nguvu hasa kutokana na umri
mkubwa.
“Tutamkumbuka sana Mzee Mandela,
amechangia kufuta uhasama baina ya watu weupe na weusi hasa kutokana na moyo
wake wa kusamehe baada ya kutoka gerezani, hivi leo suala siasa za ubaguzi
litageuka historia hasa baada ya kizazi hiki kupita,” alisema Lisa.
Nyumbani kwa Mandela, eneo la
Houghton, Mtaa wa Laan 12 jijini Johannesburg, watu kwa makundi wamekuwa
wakifika na kuweka maua kwenye vitalu vinavyozunguka makazi yake na wengine wakiandakia
ujumbe wa kumtakia heri ya kupona haraka kwenye mawe madogomadogo yaliyoko
kwenye vitalu hivyo.
Makazi hayo pia yamezungukwa na
magari yanayotumiwa na waandishi wa habari kutoka nchi mbalimbali, ambao kwa
zaidi ya wiki tatu wameweka kambi katika eneo hilo tangu kuripotiwa kuzorota
kwa afya ya kiongozi huyo.