Na Theonestina Juma, Bukoba
WATOTO wawili wakazi wa Jijini Dar ES Salaam wamefariki dunia wakati wakiogelea Ziwa Victoria eneo la gati la Kishimba mjini Bukoba.
Kamanda wa polisi Mkoani Kagera, George Mayunga alisema tukio hilo limetokea Aprili 28, jioni mwaka huu katika eneo la Kishimba mjini hapa.
Aliwataja majina ya watoto hao waliokufa maji kuwa ni pamoja na Irene Alloys (14) mkazi wa Migombani na Mariam Juma (11) mkazi wa Mbagala Jijini Dar Es Salaam.
alisema watoto hao hawakuwa na uwezo wa kuogelea na waliingia sehemu ya daraja kwenye kina kirefu ambapo kumejengwa gati la kishimba na kuzidiwa na maji na kufariki.
Alisema mpaka sasa haijabainika watoto hao walitokaje Jijini Dar Es Salaam hadi kufika mjini Bukoba.
Halikadhalika Kamanda Mayunga alisema haijajulikana watoto hao walikuwa wanaishi kwa nani mjini hapa, wala mwenyeji wao.
Alisema uchunguzi unafanyika ili kubaini watoto hao waliletwa na nani kwa malengo gani ama kama walikuwa wenyewe walitumwa na wazazi wao ama vipi.
Hata hivyo, habari zaidi zinaeleza kuwa vifo vya watoto hao viligunduliwa na Mwenyekiti wa mtaa wa kastam mjini hapa.
Habari hizo zinadai kuwa Mwenyekiti huyo ambaye jina lake halijajulikana mara moja alifanikiwa kuopoa mwili wa mtoto mmoja akisaidiana na baadhi ya wananchi na kisha kutoa taarifa kituo cha polisi Bukoba.
Taarifa zilizopatikana kuhusiana na watoto hao zimedai kuwa walitoroka kutoka jijini Dar-es-salaam wakiwa na mtoto mwingine wa kiume kwa sababu ambazo hazijafahamika na kupelekwa na wasamaria wema katika kituo kikuu cha polisi.
Kutokana na kutokuwa na mahali pa kuishi wamekuwa wakiishi katika mazingira ya kituo hicho mjini Bukoba kwa takriban wiki moja hadi walipotoroka kwenda kuogelea na kukutwa na mauti hayo.
Habari hizo zilidai kuwa mtoto mwenzao mmoja wa kiume ambaye jina lake halikufahamika haraka ambaye walikuwa wametoroka naye alifuatwa na baba yake na kurudishwa jijini humo ambapo taratibu za wazazi kuwafuata watoto waliofariki zilikuwa zikiendelea.
Kamanda Mayunga ameiomba Manisaa ya Bukoba kuangalia uwezekano wa kuwazuia watu kwenda katika eneo hilo la Kishimba kuogelea kutokana na kuwa kina kirefu na kimekuwa kikuwa watu.
mwisho
No comments:
Post a Comment