Na Theonestina Juma, Bukoba
OPERESHENI kimbunga awamu ya pili
inayoendelea katika baadhi ya mikoa ya Kanda ya Ziwa imefanikiwa kuwanasa
majambazi 88,miongoni mwao watano wamebainika kujishughulisha na biasharaya
kulanguzi wa silaha kutoka katika mnada wa nchi jirani kwa sh. 300,000 na
kuingiza nchini na kuuza kwa mamilioni
ya fedha.
Hayo yamebainishwa leo na Naibu
Kamishina wa Operesheni Kimbunga, Simon Sirro wakati akizungumza na waandishi
wa habari mjini Bukoba juu ya maendeleo
ya opereheni hiyo inavyoendelea hadi hivi sasa.
Kamanda Sirro alisema jumla ya
majambazi 88 wamekamatwa katika zoezi hilo miongoni mwao watano ni
wanaojihusisha na biashara ya kwenda nchini jirani ya Burundi kulangua silaha
hizo kwa sh.300,000 na kuingiza nchini na kuziuza kuanzia sh. milioni 1.5 na
kuendelea kwa bunduki aina ya SMG.
Halikadhalika miongoni mwa hao
watano watatu wamebainika kujihusisha katika usambazaji wa silaha hizo kwa
wateja humu nchini ambapo majambazi hao wote wamebainika kuwa ni Watanzania.
“Kuna jambazi mmoja ambaye ni Raia
wa Tanzania yeye awali alikuwa akifanya biashara ya kuuza mbuzi nchini Burundi
baada ya kuwalangua kutoka humu nchini, lakini baadaye alishawishia na watu
wengine kuwa biashara ya mbuzi halilipi bali biashara ya kuuza silaha ndiyo
inalipa naye akajiunga katika shughuli hiyo”alisema Kamanda Sirro bila kuwataja
majina yao.
Alisema katika operesheni hiyo,
awamu ya pili ilioanza Septemba 21 hadi Oktoba mosi mwaka huu, wamefanikiwa
kuwakamata wahalifu 529 wahamiaji haramu
wakiwa ni 425 kutoka katika mikoa ya Geita, Kigoma na Kagera.
Alisema wahamiaji haramu waliorushwa
kwa maamuzi ya mahakama ni 159,
waliorudishwa kwa hiari ni 122, walioachiwa huru 39 huku wanaoendelea kuhojiwa
wakiwa ni 105.
Alisema kati ya wahamiaji haramu hao
waliokamatwa, Wanyarwanda ni149,
Warundi180, Kongo 14, Waganda 82,
Pia watu watano wanashikiliwa kwa
tuhuma ya kutorosha na kuwahifadhi wahamiaji haramu pamoja na majamngili 11.
Halikadhalika silaha mbali mbali
zipatazo 23 zimekamatwa ambazo ni pamoja na SMG 3,pistol 2, magobole 18, risasi
484 za bunduki aina ya SMG/SAR zikiwa ni
471 na pistol 13, magazine mbili na bomu
la kutupwa kwa mokono likiwa ni moja na sare moja ya jeshi la nchi jirani ya
Burundi.
Katika hatua nyingine Kamanda Sirro
alisema ng’ombe 2,220 wamekamatwa ambapo ng’ombe 103 mali ya Bw. Kalemela George wilayani Biharamulo imeamuriwa na
mahakama kutaifishwa baada ya kuwangiza
katika hifadhi ya taifa Biharamulo kinyume cha sheria na hivyo kutoa wito kwa
wanaofanya biashara ya nyama mkoani Kagera kwenda kununua kwa ajili ya kuchinja na kuuza.
“Hatua hii ya kutaifishwa na
serikali hao ng’ombe itakuwa na matokeo katika jamii, hivyo wale wanaouza nyama
mabuchani wanaohangaika kutafuta ng’ombe wa kuchinja kwa ajili ya kupata nyama
ya kuuza wasisite kwenda wilayani Biharamulo kununua ng’ombe”alisema.
Alisema ng’ombe wanaobaki bado
wanafanya utaratibu wa kufikisha kesi zake mahakamani ili nao waweze
kutaifishwa.
Kwa upande wa Kaimu Mkuu wa Mkoa
Kagera ambaye pia ni Mkuu wa wilaya ya Missenyi, Kanali Issa Njiku akizungumzia
juu ya zoezi hilo alisema zoezi hilo bado linaendelea na ni endelevu na kwamba
linaenda kiawamu na hivyo wanaodhani
kuwa zoezi hilo limekwisha wanajidanganya.
Alisema ni wajibu wa wanannchi
kuendelea kutoa ushirikiano kwa maofisa wanaofanya kazi ya kuwatafuta
majangili, majambazi, wahamiaji haramu kutoa ushirikiano kwao.
Mwisho.